Wenyeviti wa Mitaa takribani 175 kutoka Kata 18 za Halmashauri ya Jiji la Mwanza wamepatiwa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao wanapowatumikia Wananchi.
Akifungua mafunzo hayo Disemba 18, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe Amina Makilagi ameanza kwa kuwapongeza Wenyeviti hao bila kujali itikadi ya vyama vyao na kusema, “ Kwanza Kabisa nawapongeza wenyeviti wote mlioaminiwa na wananchi, nilikuwa nikifuatilia mchakato mzima wa uchaguzi, kwa kweli Uchaguzi ulikwenda vizuri kwa amani bila changamoto yoyote ndiyo maana leo mko hapa, hongereni sana”.
Makilagi amewataka wenyeviti wa mitaa kutekeleza majukimu yao kwa kufuata misingi yote ya sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kati yao na wananchi badala yake waibue miradi na fursa mbalimbali zitakazopelekea maendeleo ndani ya mitaa yao.
Ameongeza kuwa kazi ya wenyeviti wa mitaa ni kuhakikisha wanawaongoza na kuwasimamia wananchi katika shuguli mbalimbali za kijamii pamoja na kuwaletea maendeleo hivyo hawapaswi kuwa chanzo cha migogoro.
“Uongozi unahitaji busara na kuridhika na hali ya maisha uliyonayo kazi ya kuuza viwanja siyo kazi ya mwenyekiti wa mtaa, ndio maana huwa mnasababisha migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikileta kero kwa wananchi mnaowahudumia” amesema Makilagi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Witness Malero amewaomba wenyeviti kuzingatia maadili ya kazi wakati wote wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Tafiti, Shauri Elekezi na Mafunzo ya Muda Mfupi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma, Bahati Mfungo amesema mafunzo hayo hiyo ni muhimu kwa wenyeviti wa mitaa kwa kuwa yatarahisisha utekelezaji wa mambo mbalimbali yanaendelea katika mitaa yao na kujifunza vitu vipya ambavyo vinakuwa vimebadilika hasa katika sera na miongozo mbalimbali inayotumika katika uongozaji na usimamiaji wa mitaa
Kwa upande wa wenyeviti Bw. Machoke Mwita ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani na Bi Zainabu Alphani wa Mtaa wa Karuta wameipongeza serikali kwa kuandaa mafunzo hayo na kusema kuwa yatawasaidia kufanya kazi zao vizuri kwa kushirikiana na wananchi katika shughuli zote za maendeleo.
Mada mbalimbali zilizowezeshwa kwa Wenyeviti hao ni pamoja na Sheria za uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Muundo, majukumu na Madaraka ya vijiji/Mitaa,na Vitongoji, Uongozi na utawala bora , Uendeshaji wa vikao na mikutano katika ngazi za Vijiji/mitaa na vitongoji, Uibuaji, upangaji na usimamizi wa miradi Shirikishi ya kijamii, Usimamizi na udhibiti wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Usimamizi wa ununuzi, Usimamizi wa Ardhi na udhibiti wa uendelezaji Miji na pamoja masuala mtambuka.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.