IDARA YA MIFUGO NA UVUVI JIJI LA MWANZA
Utangulizi
Idara ya Mifugo na Uvuvi ni miongoni mwa Idara muhimu za Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Idara hii inafanya kazi zake kwa kuakisi Dira na dhima ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo nia yake kuu ni kuinua maisha ya wananchi kwa kutoa huduma bora na kuinua uchumi wa wananchi katika Jiji la Mwanza na Taifa kwa ujumla.
Idara hii imeundwa na sekta mbili tu ambazo ni:
i. Sekta ya Mifugo
ii. Sekta ya Uvuvi
Kazi za Idara ya Mifugo na Uvuvi
Miongoni mwa kazi za Idara ya Mifugo na Uvuvi ni kama ifuatavyo;
1. Kuhakikisha usalama wa chakula na lishe bora unakuwepo katika ngazi ya kaya,
2. Kuwajengea uwezo wafugaji juu ya ufugaji bora,
3. Kuboresha miundo mbinu ya Mifugo na Samaki kwenye kata husika,
4. Kusimamia kanuni za ufugaji bora ili kuhakikisha kuwa wafugaji wanazalisha kwa tija ukilinganisha na mifugo na maeneo waliyonayo.
5. Ukusanyaji wa mapato yatokanayo Machinjio na Vyanzo vingine vya mapato idara ya Mifugo na Uvuvi.
6. Kuboresha Mifugo,Samaki na mazao yake kwenye maeneo husika,
7. Kutoa elimu ya ugani kwa wafugaji wa Mifugo na samaki,
8. Kuhakikisha usalama wa chakula na lishe bora unakuwepo katika ngazi ya kaya,
9. Kuboresha miundo mbinu ya Mifugo na Uvuvi kwenye Kata husika,
10. Kusimamia sheria na kanuni za Mifugo na Uvuvi.
Taratibu za kupata huduma
Idara inao watumishi katika ngazi mbili katika utoaji wa huduma kama ifutavyo:-
i. Ngazi ya kata ( maafisa ugani kata)
ii. Ngazi ya makao makuu ( Mkuu wa Idara na wakuu wa vitengo)
Ngazi ya kata
Katika utoaji wa huduma kwa wadau wa Mifugo na Uvuvi ambao ni wafugaji,Maafisa ugani wana madaftari ya wafugaji katika maeneo yao ya kazi. Aidha wataalamu wana ratiba zao za kazi ambao ni utaratibu wa kazi zao za kila siku. Ratiba hizo huwezesha kuwatembelea wafugaji wao hususani Majumbani na mashambani kwa ajili ya kutoa huduma za ugani. Muda huo hutoa maelekezo , ushauri, pia kusimamia kanuni za ufugaji bora kulingana na mifugo wanayonayo.
Ngazi ya makao makuu
Huduma inayotolewa na wataalamu walioko makao makuu ni masuala ya utawala. Sambamba na hilo kupokea na kutatua masuala ya utaalamu kuhusiana na Mifugo na uvuvi, yanapokuwa yamekosa ufumbuzi yanapelekwa kwenye vituo vya utafiti ili kuhakikisha kwa shughuli za Mifugo na Uvuvi. zinaendelea bila kukwama.Pindi tu utatuzi au majibu yanapopatikana yanapelekwa kwa wataalamu ngazi ya kata ili yafikishwe kwa wafugaji ili wafanikishe shughuli zao.
Shughuli zote hizi zinafanyika chini ya mkuu wa Idara ambaye ndie mwenye kuratibu mambo yote na mambo mengine yanayohusu Mifugo na uvuvi.
Miradi
Idara inao mradi mkubwa mmoja ambao ni:-
1.0 Mradi wa uboreshaji wa Machinjio ya Jiji la Mwanza
Mradi huu umeanza utekelezaji Januari, 2016 na mwisho wa utekelezaji ni July 2017. Eneo la machinjio lina ukubwa wa mita za mraba 135,000 na mahitaji ya kitoweo cha nyama yanaongezeka kila siku.
Kwa sasa wanachinja wastani wa ng’ombe 200, mbuzi 80 na kondoo 50 kwa siku. Ingawa Machinjio inategemewa sana na Jiji, haikuwa inakidhi ubora wa mazingira yake kutokana na kukosa miundo mbinu ya kudhibiti maji taka na taka ngumu hali iliyopelekea uchafuzi wa hewa na kijito kilichopo karibu kinachoungana na mto Nyashishi unaomwaga maji yake ziwa Victoria.
Hali hii imepelekea machinjio kuwa ni chanzo cha uchafuzi wa ziwa Victoria (point source pollution)
2.0 Shughuli za mradi
2.1. Ukarabati wa machinjio ya Jiji la Mwanza
2.2. Ujenzi wa mfumo wa kutibu maji taka ya machinjio ya Jiji la Mwanza (Ardhi oevu jengwa iliyounganishwa na mtambo wa kuzalisha nishati ya gesi - Bio digester)
3.0 Ukarabati wa machinjio ya Jiji la Mwanza
1. Muda wa utekelezaji: 22/07/2016 – 07/04/2017. Kuna maombi ya ongezeko la muda ili mkandarasi aweze kukamilisha shughuli zilizobaki za ufungaji wa baadhi ya vifaa vilivyoagizwa nje ya nchi.
2. Eneo la utekelezaji: Nyakato, Jiji la Mwanza
3. Wanufaika wa Mradi: Wakazi wa wilaya za Nyamagana na Ilemela
4. Watekelezaji: Halmashauri ya Jiji la Mwanza
5. Lengo: Kukarabati Machinjio ili kutengeneza mfumo wa kukusanya maji taka (ili yaingizwe kwenye mfumo wa kuyatibu) na kuboresha huduma na ubora wa nyama
6. Gharama za Mradi: Gharama kuu 980,988,900/= ambayo inafadhiliwa na LVEMP II
7. Maelezo Mafupi ya Mradi:
Mradi huu umelenga kuboresha usafi wa mazingira, huduma na ubora wa nyama kwa watumiaji. Moja ya changamoto kubwa iliyokuwepo kabla ya ukarabati ni uchafuzi wa mazingira katika eneo la Machinjio na pia ziwa Victoria kupitia mto Nyashishi ambao hupokea taka kutoka machinjio. Hii ilisababishwa na kutokuwepo mfumo wa kutibu maji taka, mtambo wa kuteketezea wanyama na nyama zilizoonekana hazifai kwa matumizi na upungufu wa matanki ya kuhifadhi maji kwa matumizi ya machinjio. Hali ya machinjio ingeweza kuhatarisha afya ya jamii inayokaa karibu na eneo hilo, watumiaji wa nyama na uchafuzi wa mazingira.
Ili kukabiliana na changamoto hizi mradi huu unakarabati machinjio hii kwa maana hasa ya kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa maji taka yaweze kuelekezwa kwenye mtambo wa kutibu kabla ya kuyamwaga kwenye mazingira.
Shughuli zinazofanyika ni
1) Ukarabati wa jengo la machinjio,
2) Ukarabati wa zizi la kutunzia mifugo kabla ya kuchinjwa
3) Chumba cha kupoozea nyama (chiller room),
4) Kujenga matanki ya kutunzia maji,
5) Kujenga shimo la kutupia mabaki ya nyama isiyofaa kwa matumizi ya binadamu,
6) kujenga mtambo wa kuchomea nyama zisizofaa kwa matumizi (Incinerator),
7) kujenga vyoo
8) kujenga jengo la ofisi.
Ukarabati huu utasaidia kupunguza uchafuzi wa maeneo ya machinjio na ziwa Victoria vilevile utaimarisha usafi na usalama wa afya ya wakazi na watumiaji wa nyama katika Jiji la Mwanza. Halmashauri ya Jiji itawajibika kununua baadhi ya vifaa vya machinjio ambavyo sio sehemu ya ufadhili wa LVEMP II.
Mpaka sasa ukarabati wote wa machinjio umekamilika kwa asilimia 95% kama inavyooneshwa katika jedwali hapa chini.
4.0 Ujenzi wa mfumo wa kutibu maji taka ya machinjio ya Jiji la Mwanza -Ardhi oevu jengwa (artificial wetland) iliyounganishwa na mtambo wa kuzalisha nishati ya gesi - Bio digester
1. Muda wa utekelezaji: Miezi 5 (Novemba 18,2016 - Machi 28,2017)
2. Eneo la utekelezaji: Machinjio ya Nyama, Mhandu, Jiji la Mwanza
3. Wanufaika wa Mradi: Wananchi wa jiji la Mwanza na bonde la ziwa Victoria kwa ujumla wake.
4. Watekelezaji: LVEMP II
5. Lengo: Kutengeneza mfumo wa kusafisha maji taka yanayozalishwa na machinjio
6. Gharama za Mradi: Gharama kuu Tshs 755,020,129 ambazo zitatolewa na LVEMP II
7. Maelezo Mafupi ya Mradi:
Mradi huu unalenga kutibu maji taka ambayo yanazalishwa na machinjio ya nyama. Shughuli za mradi huu zinahusisha usanifu (Designing), kujenga na kutoa mafunzo kwa wafanya kazi watakaoendesha na kusimamia mfumo unaojengwa wa kutibu maji taka na bio digester. Mfumo huo utawezesha kutengeneza gesi ya kibayolojia ambayo itakuwa ni njia nyingine mbadala wa nishati katika machinjio ikiwa ni pamoja na kufua umeme kwa kutumia jenereta maalum. Inatarajiwa kwamba kiasi cha mita za ujazo 319 za biogas zitazalishwa kutoka mfumo huo na itatumika katika shughuli za uchemshaji ndani ya machinjio na hivyo kuipunguzia Halmashauri ya Jiji la Mwanza gharama ya umeme. (Hapa uchafu unafanyika kuwa rasilimali ya kuzalisha nishati ya biogas badala ya kugharamia kutibu maji taka bila faida). Mfumo huu utapunguza uchafuzi wa mazingira. Halmashauri ya Jiji itawajibika kununua jenereta ya biogas ya kufua umeme kwani hiyo siyo sehemu ya ufadhili kutoka LVEMP II.
MCHANGO WA HALMASHAURI KATIKA UJENZI WA MACHINJIO HIYO
Katika kufanikisha ujenzi wa machinjio hiyo Halmashauri imechangia kiasi cha Tsh.223,039,301.32 kwa mchanganuo ufuatao.
1) Kujenga machinjio ya mbuzi amabayo inatumika kuchinjia mifugo yote wakati tumepisha ukarabati mkubwa. 148,600,000/-
2) Kulipa kazi ya tathimini ya mazingira (EIA) 49,760,000/=
3) Kununua transphomer ya umeme ya Tanesco ili kupata umeme wa njia tatu (Three phase) ili kuendana na mahitaji makubwa ya umeme kutokana na mashine zilizowekwa. 24,677,301.32
4) Kutoa huduma ya usimamizi wa mradi kwa wahandisi na wataalamu wengine wa Halmashauri.
MAFANIKIO YATAKAYO PATIKANA KWA KUKAMILIKA KWA UJENZI WA MACHINJIO.
1) kupata mapato zaidi bilioni 1 kwa mwaka kutokana na ushuru wa Ng’ombe kutegemea kupanda hadi tsh 10,000 na Mbuzi/Kondoo tsh 5000 kila mmoja (huduma ya uchinjaji na huduma nyingine.mfano kama damu n.k). Kwa sasa ushuru wa uchinjani ni mdogo sana kiasi cha (tsh. 2500/- kwa ng’ombe,Mbuzi/Kondoo tsh 1500 kila mmoja) ukilinganisha na Machinjio bora za Dodoma ushuru ni tsh. 21,500 na Arusha 13,500 kwa Ng’ombe, ambapo Mbuzi/Kondoo ni tsh 5000 kila mmoja.
2) kuzalisha nyama iliyobora ambayo itaweza kuuzwa hata nje ya nchi na kupata nyama bora hata kwa jamii ya watanzania.
3) Kuonzeza uzalishaji na thamani ya nyama itakayozalishwa pamoja na mazao yake ambayo ni Ngozi,Damu,Pembe ,Mifupa na nk
4) Ongezeko la biashara ya mifugo toka kwa wafugaji wa maeneo ya Mwanza na mikoa jirani kutokana na uwepo wa mahitaji ya mifugo katika machinjio hiyo na kuboresha maisha kwa wakazi wake.
5) Kuhifadhi mazingira katika hali ya usafi kutokana na kuboresha kwa miundombinu ya usafi na matumizi ya biogesi katika machinjio.
6) Kupatikana kwa nishati mbadala ya umeme kutokana na biogesi itakayozalishwa machinjioni na kupunguza gharama za malipo ya umeme wa TANESCO.
7) Kupatikana kwa ajira kwa wahudumu na wataalamu watakao simamia machinjio hiyo.
KAZI AMBAZO ZINATARAJIWA KUFANYIKA NA HALMASHAURI.
a) kuweka uzio wa eneo lote la machinjio ili kulinda miundombinu iliyojengwa.
b) Kuweka vifaa vya kisasa vya ndani ya machinjio (mashine) vitavyoboresha huduma ya uchinjaji na ubora wa nyama.
c) Kununua generator itayotumika kufua umeme kutoka kwenye biogas
d) Kujenga uzio wa ndani eneo la bwawa/mtambo wa kusafisha maji taka (biogesi)
e) Kujenga mabanda ya kukaushia ngozi zinazozalishwa hapo machinjioni.
f) Kuezeka sehemu ya eneo la kutunzia mifugo wakati ikisubiri kuchijwa.
4.0 HITIMISHO
Ni matarajio yetu baada ya mradi kukamilika tutakuwa tumepunguza kiasi kikubwa cha uchafuzi wa mazingira katika bonde la ziwa Victoria. Kuongeza kipato katika Jiji na kuboreha ubora wa nyama na mazao mengine ya mifugo.
Mwisho tunapenda kuwashukuru Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia mradi wa LVEMP II kuweza kutufadhili miradi wenye thamani ya tsh. 1,736,009,029/- katika ukarabati wa machinjio na miundombinu miningine kwa lengo la kudhibiti uchafuzi wa bonde la ziwa Victoria.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.