Halmashauri ya Jiji la Mwanza imepata fursa ya vijana wake 75 kunufaika na Programu ya Uwezeshaji Vijana (Work Readiness Program – WRP), inayolenga kuwaandaa kwa ajira na ujasiriamali katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Programu hiyo, inayotekelezwa na Chuo cha Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Nyegezi, imezinduliwa rasmi jijini Mwanza na itadumu kwa miezi minne. Mafunzo hayo yatawajengea washiriki ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira, sambamba na kuwahamasisha kuanzisha biashara endelevu katika sekta ya uvuvi.
Kwa mujibu wa FETA, mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za kutekeleza sera ya Serikali ya Tanzania ya kukuza ajira kwa vijana na kuimarisha maendeleo ya ujuzi. Washiriki 150 wanashiriki katika programu hii, wakiwemo vijana 75 kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, waliochaguliwa kwa ushirikiano wa karibu na uongozi wa halmashauri hiyo.
Programu hii inatekelezwa chini ya mradi wa INCLU-CITIES unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Enabel Tanzania, ikilenga sekta mbalimbali ikiwemo uvuvi, kilimo na ujasiriamali.
Sehemu kubwa ya mafunzo hayo itakuwa ya vitendo katika mashamba matano ya samaki yaliyopo jijini Mwanza, ambapo vijana watapata ujuzi wa moja kwa moja kuhusu ufugaji wa samaki wa vizimba, usimamizi wa mashamba, utengenezaji wa chakula cha samaki, masoko na uchakataji wa bidhaa.
Akizindua rasmi mafunzo hayo, Bi. Merisia Sebastian Mparazo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa FETA, aliwahimiza washiriki kutumia fursa hii kuongeza ujuzi na kuchochea ajira kwa vijana wa Mwanza.
"Kupitia mafunzo haya, vijana wa Mwanza watakuwa sehemu ya mabadiliko katika sekta ya uvuvi, sekta ambayo kwa sasa inachangia asilimia 1.7 ya pato la taifa na inawaajiri zaidi ya watu milioni sita nchini,” alisema Bi. Mparazo.
Kwa upande wake, Bw. Thomas Aikarua, Mtaalamu wa Elimu ya Ufundi Stadi (TVET) kutoka Enabel, alisisitiza dhamira ya Enabel kuendelea kushirikiana na taasisi za serikali, sekta binafsi na halmashauri katika kukuza suluhisho bunifu za kijani zitakazoongeza ajira kwa vijana.
Chini ya mradi wa Inclu-Cities, vijana wa Jiji la Mwanza watapatiwa pia mafunzo ya ujasiriamali kupitia SIDO Mwanza, na baadaye kuandaa miradi ya biashara itakayoshindanishwa kupata ufadhili kutoka CRDB Foundation, ambayo pia ni mshirika wa mradi huu.
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetambua umuhimu wa programu hii kama kichocheo cha ajira endelevu, hasa kwa vijana wanaoishi kandokando ya Ziwa Victoria ambapo fursa za kiuchumi katika uvuvi na ufugaji wa samaki ni nyingi.
Kwa mujibu wa uongozi wa Halmashauri, mpango huo utasaidia kuinua kipato cha kaya, kukuza uchumi wa kijani na kuimarisha mchango wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya jiji na taifa kwa ujumla.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.