Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Nyamagana Leo Januari 29,2026 kwa lengo la kukagua na kuweka Jiwe la Msingi katika ujenzi wa Shule mpya ya sekondari inayojengwa kwa mfumo wa ghorofa mtaa wa Kasota kata Mhandu.
Mhe. Mtanda akizungumza katika hafla hiyo ameipongeza serikali kwa kuendelea kutoa fedha za miradi katika kutekeleza miundombinu ya elimu kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza huku akiweka bayana kuwa” kuanzia mwaka 2021 hadi sasa kumekuwa na ongezeko la shule za sekondari 58”
Vilevile amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoa fedha kiasi cha Tshs milion 200 ili kuharakisha ujenzi wa shule hiyo ili ifikapo Januari 2027 wanafunzi wa kidato cha kwanza waanze Mara moja ili kusaidia kupunguza msongamano.
Kwa upande wake Mhe. Amina Makilagi Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miundombinu ya elimu ambapo amesema ujenzi wa shule hii utagharimu jumla ya kiasi cha Tshs Bilioni 4.6 na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 1620 na kufanya mtaa wa Mhandu kuwa na Shule mbili za sekondari hivyo itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Mhandu Mwl. Warioba Marato akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa ameeleza ujenzi ulianza juni 2025, na serikali ilitoa kiasi cha Tsh. 584.2 kwa lengo la kujenga shule ya sekondari ya kawaida katika kata hiyo lakini kutokana na ufinyu wa eneo na ongezeko la wanafunzi kuwa kubwa Halmashauri uliamua shule hiyo ijengwe kwa mfumo wa Ghorofa.
Mwl. Marato ameongeza kuwa mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 45% na ili ujenzi kukamilika unahitaji Bilioni 1.56 huku akiweka bayana kuwa kwa mwaka 2026 wanafunzi waliyochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni 13,609 na waliyokwisha kulipoti ni 10,195 Sawa na asilimia 75.03% ya wanafunzi wote waliyopo shuleni.
Aidha Msitahiki Meya wa Jiji la Mwanza Mhe. Sima Costantine Sima amesema shule Hii ni ya kimkakati na itasaidia kuhudumia mitaa zaidi ya saba katika kata ya Mhandu na mitaa minne ya jirani iliyopo kata ya igoma hivyo kusaidia kupunguza msongamano na wanafunzi kutotembea umbali mlefu kutafuta elimu.
Shule hiyo pindi tu itakapokamilika itaitwa Said Mtanda sekondari ikiwa ni kumbukizi yakuyaenzi mazuri anayoyatenda na kuyatekeleza kwa kuchapa kazi huku akichochea Maendeleo ya Mkoa wa Mwanza katika miundombinu mbalimbali ikiwemo Sekita ya elimu.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.