Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi, ameitaka jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti, ikiwa ni njia ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Makilagi ametoa wito huo leo Januari 27,2026 wakati wa zoezi la upandaji miti lililofanyika katika Shule ya Sekondari Kakebe iliyopo Kata ya Igoma , ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni muasisi wa kampeni ya Tanzania ya Kijani.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya amesema zaidi ya miti 2,000 imepandwa katika vituo vya Afya, zahanati na kati ya hiyo miti zaidi ya 1,200 imepandwa ndani ya Shule ya Sekondari Kakebe Leo.
Mheshimiwa Makilagi amesisitiza kuwa miti yote iliyopandwa italindwa na kutunzwa ili kuhakikisha inanawiri na kuleta tija iliyokusudiwa, ikiwemo kuboresha mazingira, kuhifadhi vyanzo vya maji na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
„Tunapanda miti kuondoa hewa Ukaa na kupata mazingira wezeshi yakufundishia huku tukiendeleza utengenezaji wa lishe bora kwa watoto na kizazi kijacho kwa kupanda miti ya matunda hususani maparachichi“ amesema Makilagi.
Aidha, amewahimiza wanafunzi, walimu na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yao na kuitunza ili kuhakikisha kampeni ya Tanzania ya Kijani inaleta matokeo chanya kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika Hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefanikisha kutatua changamoto ya umeme na maji vinavyogharimu takribani shilingi 1,800,000 ambapo amefanya harambee na kupata kiasi cha shilingi 1,350,000. Huku akimuagiza meneja wa Tanesco kutoa Control namba na umeme uje Mara moja katika shule hiyo ya sekondari Kakebe na kumtaka Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuongeza kiasi kilichobaki ili kumaliza changamoto ya maji kwa haraka.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.