Afisa Madai Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Blasius R. Lombo, ametoa mafunzo rasmi kwa watumishi wa Halmashauri kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko huu, huduma zinazotolewa, na mafao wanayostahili wanapopata changamoto kazini. Elimu hiyo imetolewa leo Septemba 16, 2025 katika ukumbi mkubwa wa Jiji kwa lengo la kuongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu haki zao na wajibu wa mwajiri chini ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Act, Cap. 263).
Bw. Lombo alifafanua kuwa WCF ni mfuko wa hifadhi ya kijamii unaolenga kulinda wafanyakazi pale wanapopata ajali kazini, magonjwa yanayotokana na kazi, au kifo kinachosababishwa na kazi. Alisisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kujiunga na mfuko huu mara anapoajiriwa, kwani hata baada ya kustaafu, WCF huendelea kutoa huduma na mafao kwa kipindi cha hadi miaka 12 ikiwa madhara au ulemavu uliotokea kazini bado unamathiri.
Akielezea kuhusu huduma zinazotolewa, Bw. Lombo alisema kuwa WCF hutoa huduma za matibabu ya ajali na magonjwa ya kazi, urejeshaji (rehabilitation), tathmini ya ulemavu, na msaada wa kimsingi kama matibabu yanayohitaji upasuaji au vifaa tiba. Kwa mfano, mfuko umeingia mikataba na hospitali zote za rufaa nchini, na kwa Mkoa wa Mwanza huduma hizi zinapatikana katika Hospitali ya Sokoine, Bugando, na Kamanga, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama wake.
Kuhusu mafao, afisa huyo alifafanua kuwa: Fidia ya ulemavu wa muda: Kwa mfanyakazi ambaye hawezi kufanya kazi kwa muda, WCF hulipa 70% ya mshahara wa mwezi kwa kipindi ambacho mfanyakazi hawezi kufanya kazi, hadi miezi 24.
Fidia ya ulemavu wa kudumu: Ikiwa madhara yamebaki na hayapo kwenye matarajio ya kupona, fidia inaweza kuwa mkupuo (lump sum) au pensheni ya kila mwezi, kulingana na kiwango cha ulemavu.
Fidia kwa familia/wategemezi: Kwa wafanyakazi waliopoteza maisha kutokana na ajali au ugonjwa wa kazi, familia yao inapata msaada wa kifedha na mazishi.
Huduma baada ya kustaafu: WCF huendelea kumhudumia mfanyakazi hata baada ya kustaafu kwa kipindi cha hadi miaka 12 ikiwa madhara yanayohusiana na kazi bado yanaendelea kumletea matatizo.
Bw. Lombo pia alieleza mchakato wa kuripoti ajali na madai ya fidia: mtumishi anatakiwa kuripoti ajali au ugonjwa wa kazi ndani ya miezi 12 tangu tukio lipofanyika au ugonjwa kugunduliwa. Ni muhimu kuhifadhi nyaraka zote muhimu, ikiwemo ripoti za matibabu, ushahidi wa ajira, na taarifa za madaktari ili mchakato wa malipo ya fidia uwe rahisi na wa haraka.
Aidha, afisa huyo alibainisha changamoto zinazokwamisha uelewa na usajili wa WCF, ikiwemo uelewa mdogo wa waajiri na wafanyakazi, ucheleweshaji wa malipo ya michango, na upungufu wa rasilimali za uhamasishaji hasa katika maeneo ya vijijini. Alisisitiza kuwa elimu juu ya WCF ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha kila mtumishi anajua haki zake na faida za mfuko huu.
Kikao kilimalizika kwa washiriki kupata nafasi ya kuuliza maswali na kupokea ufafanuzi wa moja kwa moja kutoka kwa Bw. Lombo, jambo lililoongeza uelewa wa wafanyakazi na kuondoa sintofahamu kuhusu mafao na huduma zinazotolewa na WCF. Watumishi walisisitiza kuendelea kushirikiana na WCF na waajiri wao ili kuhakikisha kila mmoja anapata ulinzi unaostahili kazini
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.