Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, leo Januari 29, 2026 amefanya ziara ya kikazi Wilaya ya Nyamagana na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya ghorofa mtaa wa Kasota, kata ya Mhandu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mtanda ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu akibainisha kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi sasa shule za sekondari zimeongezeka kwa shule 58 mkoani Mwanza.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutoa Tsh milioni 200 ili kuharakisha ujenzi wa shule hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaanza masomo Januari 2027.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi, amesema ujenzi wa shule hiyo utagharimu Tsh bilioni 4.6 na itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,620.
Ameongeza kuwa shule hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kufanya kata ya Mhandu kuwa na shule mbili za sekondari.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Mhandu, Mwl. Warioba Marato, amesema ujenzi ulianza Juni 2025 na umefikia asilimia 45, huku mahitaji ya fedha yaliyobaki kukamilisha mradi huo yakiwa ni Tsh bilioni 1.56.
Amebainisha kuwa mwaka 2026 wanafunzi 13,609 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, ambapo 10,195 tayari wameripoti sawa na asilimia 75.03.
Aidha, Msitahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Mhe. Sima Costantine Sima, amesema shule hiyo ni ya kimkakati itakayohudumia mitaa zaidi ya saba ya kata ya Mhandu na mitaa ya jirani ya kata ya Igoma, hivyo kupunguza msongamano na umbali wa wanafunzi kufuata elimu.
Shule hiyo ikikamilika itaitwa Said Mtanda Sekondari, ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wa Mhe. Said Mtanda katika kuchochea maendeleo ya elimu na miundombinu mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mwanza.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.