Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na watumishi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Jana tarehe 15/10/2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- TAMISEMI Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amewataka wananchi kutochanganya kati Uandikishaji Katika Daftari la Tume huru ya Uchaguzi linahusisha uchaguzi wa Rais, wabunge na Madiwani na daftari la Makazi linahusisha uchaguzi wa Wenye viti wa serikali za mitaa na wajumbe wanaounda serikali hiyo.
Aidha ameeleza kuwa zoezi linaloendelea hivi sasa linahusisha uchaguzi wa viongozi ngazi za mitaa na kwamba mtanzania yoyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea anayo sifa ya kujiandikisha na kushiriki Uchaguzi ifikapo tarehe 27 Novemba 2024 pia anayo haki ya kuchagua au kuchaguliwa.
Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha Katika daftari la Makazi ili kupata haki yao kikatiba ya kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa.
Pia Waziri amewataka viongozi wa vyama vyote 19 vitakavyoshiriki uchaguzi huo kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi juu ya uandikishaji na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu kwa kuwa ni haki yao kikatiba.
Sambamba na hilo Waziri ametoa ufafanuzi juu ya taarifa zinazosambaa kuwa TAMISEMI haijatoa elimu toshelezi kwa wananchi juu zoezi hili, kwa upande wake amesema kuwa suala la Uchaguzi lipo kikatiba na liko katika kalenda ya mwaka na kusisitiza kuwa kazi ya kutoa elimu imefanyika kwa kiwango cha juu kuanzia ngazi ya TAMISEMI hadi mtaa.
Waziri Mchengerwa amevipongeza vyombo vya habari kwa namna vinavyoshiriki Katika kutoa elimu kwa wananchi kupitia vipindi mbalimbali na kuwaomba zoezi hilo liwe endelevu ili kuwafikia wananchi wote na kuongeza kuwa zipo taasisi zaidi ya 83 zilizoko sehemu mbalimbali ambazo jukumu lao ni kutoa elimu kwa wananchi.
Vilevile ametoa ufafanuzi juu ya taarifa zinazosambaa Katika mitandao ya kijamii kuwa kuna vituo bandia, amesema kuwa taarifa hizo si za kweli na zinalenga kuvuruga zoezi la Uchaguzi
Waziri Mchengerwa amewaomba viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kufuata kanuni za uchaguzi zinazoelekeza juu ya suala zima la Uchaguzi.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.