Watendaji wa kata 18 na mitaa 175 katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza wamehimizwa kuwajibika ipasavyo katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan kwenye ufuatiliaji na ukusanyaji wa mapato ya halmashauri.
Rai hiyo imetolewa Desemba 29, 2025 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni Kibamba, wakati akizungumza na watendaji hao.
Ameeleza kuwa kila mtendaji anatakiwa kutimiza wajibu wake kwa nafasi aliyonayo ili kuhakikisha malengo ya halmashauri yanafikiwa.
Mkurugenzi amesisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa mapato akieleza kuwa kwa sasa mfumo wa Balozi System utaendelea kutumika, huku akibainisha kuwa ofisi rasmi za ukusanyaji wa mapato zitafunguliwa katika ngazi ya kata na kila kata itakuwa na meneja maalum wa kuratibu masuala ya ukusanyaji wa mapato.
Katika kuhakikisha ufanisi unaongezeka, Wakili Kibamba amewataka watendaji kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu na kuzingatia malengo yaliyowekwa.
Ameagiza kila mtendaji wa mtaa kuhakikisha anatembelea biashara zisizopungua thelathini (30) kwa siku, ili kubaini na kusimamia ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara wanaostahili kulipa..
Aidha, amebainisha kuwa watendaji wote watapimwa kwa utendaji wao wa kazi, hususan katika eneo la ukusanyaji wa mapato, na kuwataka kuwasilisha taarifa za utekelezaji kila mwezi.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bw. Mussa Mbyana, amewataka watendaji hao kuzingatia na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa. Pia amesisitiza umuhimu wa kupanga ratiba zao vizuri ili waweze kuwahudumia wananchi ipasavyo katika maeneo yao ya kazi.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.