Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni Kibamba ameongoza kikao kazi kilichowakutanisha watumishi wote wa makao makuu ya Halmashauri kwa lengo la kutoa maelekezo, maagizo, kuwakumbusha majukumu na kuhimiza uwajibikaji.
Kikao hicho kimefanyika leo Mei 8, 2025 katika ukumbi wa Gandh Hall na kusisitiza nidhamu kwa kuwa ni msingi wa kwanza wa mafanikio katika mahali pa kazi na kuongeza kuwa kila mtumishi anatakiwa kuipenda, kuiheshimu na kuithamini Kazi na nafasi alinayonayo.
“Onyesha upo, siyo kwa kuitika jina, onyesha umuhimu wako kwenye nafasi uliyonayo,” amesema Kibamba.
Vilevile Kibamba amehimiza suala la usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri na kuwataka watendaji wa mitaa kuhakikisha maeneo yote ndani ya mitaa yao yanakuwa safi sambamba na kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka sheria na kanuni za usimamizi wa mazingira.
Aidha Kibamba amesisitiza ukusanyaji wa mapato na kuelekeza kuwa kuanzia jumatatu watumishi wote watatakiwa kushiriki zoezi hilo.
“Nataka tugawane mitaa kuanzia asubuhi mpaka saa kumi jioni, tukatembelee kila Biashara tukakague leseni, biashara mpya na kodi ya huduma(service levy) kwa kutumia balozi system.” Alisema Kibamba
Kikao kilitoa fursa kwa watumishi kuelezea changamoto zinazowakabili katika mazingira ya kazi ambapo baadhi ya changamoto ni pamoja na upungufu wa vitendea Kazi ambapo Wakili Kiomoni amezipokea na kuwaagiza wahusika kuhakikisha wanashughulikia changamoto zote kwa wakati.
Katika hatua nyingine Kibamba ameahidi kumaliza kabisa changamoto ya madawati kwa shule za Msingi na Sekondari.
“ kuna changamoto kubwa ya madawati Shule za Msingi na Sekondari, kwa mwaka huu nataka na nimedhamilia kufikia Juni 30,2025 niwe nimepeleka fedha kwa ajili ya utengenezaji wa madawati yote yanayotakiwa kwa shule za Sekondari, na kwa shule za Msingi kabla ya Julai nataka kumaliza changamoto hiyo…..” amesema Kibamba
Kibamba amesisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano baina ya watumishi, ubunifu katika utoaji wa huduma na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.