Ameyasema hayo wakati akifungua semina kwa viongozi wa bodaboda mkoani Mwanza iliyoandaliwa na Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CC) Mkoa Mwanza, iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Aidha Mhe. Dkt. Nyimbi ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza amewahimiza bodaboda na watumiaji wengine wa huduma za nishati na maji kutoa taarifa pindi waonapo mtoa huduma anakiuka kanuni na sheria zinazomlinda mteja huku nao wakitimiza wajibu wao ikiwemo kulipia kwa wakati ankra na malipo mbalimbali ili kupata huduma endelevu.
Katibu Mkuu Mtendaji EWURA CC Taifa, Mhandisi Goodluck Mmari amesema lengo la semina hiyo ni kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za nishati na maji kwa kundi la bodaboda ili aweze kutambua haki na wajibu wao hatua itakayosaidia upatikanaji wa huduma bora kuelekea kwenye uchumi wa kati.
Naye mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Makoye Kayanda ambaye ni dereva bodaboda Jijini Mwanza amelishukuru Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CC) na kuongeza kwamba elimu waliyoipata itawasaidia kuongeza uwajibikaji baina ya watoa huduma na wateja.