Uzio uliojengwa kinyume cha sheria ya ujenzi umevunjwa katika Kata ya Mahina, Mtaa wa Mwananchi, kufuatia ziara ya ukaguzi iliyofanywa na timu ya wataalamu kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni K. Kibamba, Desemba 29, 2025.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wataalamu wa halmashauri kujiridhisha kuwa Bw. Chacha Masubo Surati hakufuata taratibu za ujenzi, jambo lililosababisha mgogoro wa ardhi kati yake na wananchi wa mtaa huo, kufuatia kuzibwa kwa barabara iliyokuwa ikitumiwa na wananchi tangu miaka ya 1980.
Baada ya ukaguzi wa kina na vipimo vya kitaalamu, ilibainika kuwa Bw. Chacha aliingia kwenye eneo la umma hali iliyomlazimu Mkurugenzi wa Jiji kuagiza sehemu ya uzio uliovamia barabara kubomolewa mara moja.
Aidha, Mkurugenzi aliwaagiza viongozi wa ngazi ya kata na mtaa kuhakikisha barabara hiyo inafunguliwa mara moja kwa matumizi ya wananchi, pamoja na kusimamisha ujenzi huo hadi taratibu zote za kisheria zitakapofuatwa ipasavyo.
Taarifa kutoka Idara ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilionyesha kuwa Bw. Chacha aliomba kibali cha ujenzi wa kiwanja kimoja, lakini aliamua kujenga katika viwanja vitatu vilivyofuatana, jambo lililosababisha mvutano na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Mtaa wa Mwananchi.
Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeendelea kusisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria, na imewataka wananchi wote kufuata taratibu za ujenzi na umilikishaji wa ardhi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.