Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa tano katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza.
Akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo, Katibu wa Wizara ya Afya, Mhe. Tumaini Nagwa, alisema fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani pamoja na ruzuku kutoka serikali kuu.
“Kukamilika kwa jengo hili kutasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya kwa wananchi,” alieleza Mhe. Nagwa.
Kwa mujibu wa mhandisi ambaye ni msimamizi wa mradi, Bi. Ester Shayo, tayari zaidi ya shilingi milioni 400 zimepokelewa na kutumika, huku ghorofa ya kwanza ikitarajiwa kutumia zaidi ya bilioni 1.2.
Katika ziara hiyo, Mhe. Nagwa pia alitembelea Kituo cha Afya cha Mkolani, na kufurahishwa na ufanisi wa huduma zinazotolewa. Alitoa wito kwa Daktari Mkuu kuhakikisha ujenzi wa maabara ya kisasa unaanza haraka ili kuongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa wanaofika kituoni hapo.
“Ni muhimu kuhakikisha kituo hiki kinakuwa na maabara bora kwa ajili ya kutoa huduma sahihi na salama kwa wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Bi. Khadija Juma, mmoja wa wananchi waliopokea huduma katika kituo hicho, aliishukuru serikali kwa maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya afya.
“Sasa hivi tunapata huduma ya uzazi kwa usahihi na usalama wa hali ya juu kabisa,” alisema kwa furaha.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya afya, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha huduma bora zinamfikia kila Mtanzania.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.