Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Mheshimiwa John Francisco Nzilanyingi, leo tarehe 09 Januari, 2026, amefanya ziara ya kutembelea na kujionea hali ya waathirika wa mafuriko yaliyosababishwa na Mto Mirongo katika Kata ya Mirongo, Jijini Mwanza.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mbunge aliambatana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na wataalamu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa lengo la kufanya tathmini ya athari za mafuriko hayo na kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto iliyopo.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mirongo, Mheshimiwa Nzilanyingi aliwashukuru kwa dhati kwa kumpa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na akaahidi kuendelea kusimamia na kupigania maslahi yao, hususan katika masuala ya miundombinu na usalama wa maisha ya wananchi.
Aidha, Mheshimiwa Mbunge alitoa ufafanuzi kuhusu mpango wa ujenzi wa Daraja la Masai, akibainisha kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza hivi karibuni. Sambamba na hilo, alieleza kuwa kazi ya ujenzi na uimarishaji wa kingo za Mto Mirongo itatekelezwa kuanzia Ziwa Victoria hadi eneo la Mabatini, hatua inayolenga kudhibiti mafuriko na kuondoa adha inayowakumba wananchi mara kwa mara.
Wananchi wa Kata ya Mirongo walieleza matumaini yao makubwa kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kurejesha hali ya kawaida, kulinda makazi yao, na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.