Katika jitihada za kulinda na kuhifadhi mazingira ya Ziwa Victoria, wadau wa sekta ya uvuvi, mazingira na jamii kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela wamekutana katika kikao maalum cha kujadili changamoto za taka za plastiki na nyavu zilizotelekezwa ziwani (ghost gear) zinazoharibu mazingira na kuathiri rasilimali za ziwa.
Akifungua kikao hicho January 16,2025 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bw. Oswald Mpelasoka ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Mazingira, alisisitiza kuwa lengo la kikao ni kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kulinda Ziwa Victoria na kuendeleza uvuvi endelevu unaozingatia usimamizi bora wa mazingira.
Aidha Mtaalamu wa mazingira, Dr. Bahati Mayoma, aliwasilisha mada kuhusu athari za taka za plastiki ndani ya Ziwa Victoria, akieleza kuwa plastiki zinazotupwa hovyo au kuingia ziwani kupitia mito na mifereji ya maji huchafua maji, huua viumbe wa majini na kuleta hatari za chembe chembe za plastiki ambazo zinaweza kuingia katika mlolongo wa chakula na kuathiri afya za binadamu.
Wawakilishi wa wavuvi walieleza changamoto za nyavu zilizotelekezwa ziwani kuvua samaki bila kudhibitiwa, kuharibu mazalia ya samaki na kupunguza rasilimali za uvuvi, jambo ambalo linaathiri moja kwa moja kipato na usalama wa chakula wa jamii zinazotegemea ziwa.
Hatua hii ya kukutanisha wadau imewezekana kupitia Mradi wa SASA – Green and Smart Cities unaotekelezwa katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela, ambao umewezesha ushirikiano wa wadau wa uvuvi, mazingira na jamii kuweza kubaini changamoto, kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja ya kuhifadhi ziwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Wadau walipendekeza kuimarisha elimu kwa wavuvi na jamii zinazozunguka ziwa, kuweka mifumo madhubuti ya ukusanyaji wa nyavu chakavu na taka za plastiki, pamoja na kuongezwa kwa doria za usimamizi wa uvuvi ili kuhakikisha utunzaji bora wa rasilimali hizi muhimu.
Kikao kilihitimishwa kwa wito wa ushirikiano wa pamoja kati ya wadau wote kuhakikisha Ziwa Victoria linaendelea kuwa chanzo cha maisha, maendeleo na ustawi wa jamii zinazolizunguka.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.