Siku ya Wanawake Duniani ni kielelezo cha juhudi za pamoja za kutafuta haki na usawa wa kijinsia, huku ikisisitiza kuwa jamii yenye usawa ni bora zaidi kwa maendeleo ya nchi na ulimwengu mzima.
Kwa kutambua umuhimu wa wanawake na wasichana katika jamii kama kaulimbiu ya mwaka huu isemavyo, “ Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” leo Machi 4, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amewaongoza wanawake na wasichana katika matembezi ya hisani kama ishara ya uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani itakayoadhimishwa Kimkoa Machi 6 katika Wilaya ya Nyamagana na Kitaifa Machi 8, 2025 Jijini Arusha.
Akimkaribisha Mkuu Wilaya ya Nyamagana baada ya matembezi ya hisani Bi. Zena Kapama Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza amesema kuwa Siku hii inatoa fursa ya kukumbuka na kusherehekea wanawake waliopigania haki za msingi na usawa katika jamii, tangu mwanzo wa mchakato wa harakati za wanawake.
Katika uzinduzi huo Mhe. Makilagi amesema kuwa siku hii inahusiana na mapambano ya wanawake kwa haki zao za kijamii, kisiasa, na kiuchumi pamoja na kutathmini hatua zilizofikiwa na kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha haki za wanawake zinaheshimiwa na kwamba wanawake wanapata nafasi sawa katika jamii.
Uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika Wilaya ya Nyamagana yameambatana na Bonanza ambapo maonyesho mbalimbali yameipamba siku hii ikiwemo, mbio za mita Mia, mpira wa Miguu, mpira wa Pete, kukimbiza kuku, kukimbia kwenye gunia na mingine mingi.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.