Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) ni njia moja wapo ya kukuza na kuboresha Elimu Nchini. Kwa kutambua hilo Afisa Elimu wa Awali na Msingi Bw. Mussa Ally Lambwe ameendesha Mafunzo kwa walimu mahiri wa KKK (3R’S) kwa shule za Msingi za Serikali na binafsi.
Akifungua mafunzo hayo March 25,2025 katika ukumbi wa Lake Victoria English Medium, Bw. Lambwe amesema lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo walimu hao katika nyanja tofauti wakati watakapokwenda kutekeleza majukumu yao katika ngazi ya Shule.
Ameongeza kuwa Kamati ya Mitihani ya Wilaya ilifanya tathmini kupitia mtihani wa Taifa darasa la pili 2023 na kubaini changamoto zilizosababisha baadhi ya wanafunzi kutomudu kujibu vizuri katika stadi lengwa hivyo kuamua kufanya mafunzo hayo ili kutoa mbinu za ziada zinazoweza kusaidia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika darasa.
Kwa upande wake Mwl Sauda ambaye ni mwezeshaji na mbobezi wa masuala ya Awali, darasa la kwanza na la pili amebainisha changamoto zilizojitokeza kuwa ni baadhi ya wanafunzi kushindwa kuandika, kuchanganya herufi kubwa na ndogo pia mwendokasi katika kasi ya kusoma.
Mwl Sauda ameongeza kuwa kupitia mafunzo haya walimu wataweza kutatua changamoto zote zilizojitokeza na zitakazojitikeza kwa kutumia mbinu rahisi na wezeshi wakati wa tendo la ufundishaji.
“Sisi kama wawezeshaji tumeamua tuwape hizo mbinu, tuwawezeshe walimu wetuwaweze kujua njia/mbinu rahisi za kuweza kumfundisha Mtoto aweze kung’amua mambo mbalimbali kwa haraka”.
Kwa niaba ya wawezeshwaji Mwl Aneth Kessy amesema ,“ Tunaishukuru Halmashauri yetu kwa jitihada nzuri kama hizi, tunaahidi kupitia mafunzo haya tunakwenda kufanya mabadiliko katika stadi za KKK”.
Afisa Elimu wa Awali na Msingi Bw. Lambwe ametamatisha kwa kuwashukuru washiriki wote na kuwataka wawezeshaji kuhakikisha walimu wote wa stadi za KKK wanashiriki kikamilifu mafunzo ngazi za shule ili kuleta tija na ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.