Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Mheshimiwa John Francisco Nzilanyingi, leo Januari 6,2026 amekutana na Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa lengo la kufahamiana pamoja na kueleza dhamira na mwelekeo wake wa utekelezaji wa majukumu ya ubunge kwa kipindi cha miaka mitano kwa wananchi wa Nyamagana.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Nzilanyingi aliomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa Menejimenti ya Halmashauri, akisisitiza kuwa watendaji wa Serikali ndio mhimili muhimu wa kutafsiri Ilani ya Chama Tawala kwa vitendo na kuifikisha kwa wananchi.
“Nyie watendaji ndio watu sahihi wa kuitafsiri Ilani ya Chama kwa vitendo kwa wananchi,” alisisitiza Mbunge Nzilanyingi.
Aidha, Mbunge huyo alisema kuwa muda si mrefu ataanza ziara katika maeneo mbalimbali ndani ya Jimbo la Nyamagana, ambapo ataambatana na wataalamu wa Halmashauri kulingana na changamoto za maeneo husika, ili kuhakikisha suluhisho la changamoto hizo linapatikana kwa ufanisi.
Mheshimiwa Nzilanyingi pia alihimiza kila kiongozi na mtumishi wa umma kuacha alama chanya katika eneo analolisimamia kwa kuwahudumia wananchi kwa bidii, uwajibikaji na uadilifu.
Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni Kiburwa Kibamba, alisema Menejimenti ipo tayari kutoa ushirikiano wa karibu na kumwezesha Mbunge wa Nyamagana kufanikisha malengo na ndoto zake kwa manufaa ya wananchi.
“Kauli mbiu ya TAMISEMI ni kuwapatia wananchi tabasamu. Hii ina maana ya kuwahudumia wananchi kwa weledi, kutatua changamoto na kero zinazowakabili wananchi,” alisema Mkurugenzi Kibamba.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.