Maadhimisho ya siku ya afya na lishe wilayani Nyamagana yamefanyika leo tarehe 23/09/2023 yakiwa yamebeba dhima ya utoaji elimu kwa jamii juu ya afya na lishe kwa mtoto kuanzia kipindi cha mimba hadi mtoto anapofikia miaka miwili yaani siku 1000.
Akitoa elimu kwa wanajamii wa mtaa wa Majengo, Mganga mkuu wa Jiji Dkt. Sebastian Honorati Pima amewaeleza wanajamii kuwa jamii inapaswa kuwa makini na suala la lishe tangu mama anapokuwa mjamzito hadi anapojifungua na hata mtoto anapofikisha miaka miwili sawa na siku elfu moja(1000) kwa kuwa kipindi hiki ubongo wa mtoto unakuwa unaendelea kutengenezeka na ni muhimu kwa malezi na makuzi ya mtoto ili aweze kuwa mbunifu na afya njema.
Akizungumza na wanajamii hao Dkt. Pima amesema, “bila ya kuwa na lishe nzuri kwa watoto na jamii kwa ujumla tutatengeneza jamii yenye watu wenye udumavu wa ubongo na ya kwamba kutozingatia lishe bora katika kipindi hiki cha siku 1000 tutazalisha watu wasioweza kupambanua mambo na kufanya maamuzi sahihi kwa taifa letu.” Amesema hayo Dkt Pima.
Aidha katibu tawala wa wilaya ya Nyamagana,Ndg. Thomas Salala amesisitiza jamii kuzingatia elimu inayotolewa juu ya suala zima la afya na lishe kwani kupitia elimu hii itaisaidia jamii kuzalisha wanajamii wenye afya bora,uelewa mzuri wa mambo mbalimbali na hivyo kuchangia taifa kuwa na wanajamii na viongozi bora kwa maendeleo ya taifa letu.
Naye Afisa Lishe wa Wilaya ya Nyamagana Ndg. Joyce Zelamula amefafanua namna nzuri ya uandaaji wa uji lishe wenye virutubisho mbalimbali na namna ya uchanganyaji wake kwenye chakula cha mtoto.Akifafanua kwa mfano dhahiri wa uandaaji uji lishe, amesema,”mtoto anapokuwa mdogo ndipo ubongo wake unatakiwa kupata vyakula bora venye virutubisho bora ili mtoto huyo awe na afya njema,makuzi bora na akili yenye kumbu kumbu nzuri.” Amefafanua Ndg. Joyce.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.