Hayo yamebainishwa mapema leo Septemba Mosi wakati wa ziara ya Kamati ya siasa Mkoa wa Mwanza walipotembelea mojawapo ya mradi mkakati unaotekelezwa wa ujenzi wa soko kuu la kisasa la mjini kati katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
"Mimi binafsi nimeridhishwa sana na mpangilio wa mradi huu ni jumuishi umegusa makundi karibu yote kuna sehemu ya machinga na mama lishe na uwekezaji huu unakwenda kuifanya mwanza kuwa ya kisasa na kuifananisha na majiji mengine." Amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima ambaye pia ni Kamisaa wa Kamati ya siasa Mkoa.
Mhe Malima emeongeza kuwa mradi huu mkubwa unaogharimu zaidi ya Bilioni 20 hadi kukamilika kwake una nia ya kuhamisha maisha ya wananchi kwenda kuwa ya kisasa na kutoa rai kwa halmashauri, huduma zitakazotolewa ma soko hili ziwe zilenge kuwasaidia wananchi hasa wafanyabiashara wadogo ambao Mhe. Rais amekua akiwahangaikia."
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Ndg. Erick Mvati amefafanua kuwa mradi huu ambao umeanza Oktoba 2020 na unatarajia kukamilika ifikapo Septemba 30, 2022 unagharimu zaidi ya Tshs. Bilioni 20 hadi kukamilika kwake na kwa sasa umefikia asilimia 79 ya utekelezaji.
Aidha, amefafanua kuwa Mradi huo ulioajiri zaidi ya vijana 100 wakati wa utekelezaji, utasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri na kupunguza utegemezi kutoka Serikali kuu kutokana na huduma kadhaa zitakazokuwemo zikiwemo mabenki, vizimba vya wafanyabiashara wadogo, eneo la wafanyabiashara wakubwa, michezo ya watoto na eneo la kuegesha magari zaidi ya 150.
Ikiwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilaya ya Nyamagana, Kamati imepata nafasi pia ya kupita na kukagua bandari ya Mwanza Kusini na kukagua Ujenzi wa Meli kubwa ya kisasa ya MV Mwanza ambayo inatekelezwa na Mkandarasi Gas Entec ya Nchini Korea kwa Bilioni 70 na imesisitiza uharakishwaji wa ujenzi huo kwa manufaa ya wananchi waishio kwenye ukanda wa maziwa makuu.
"Ujenzi wa hii Meli ulianza January 2019 na ulikua uende kwa miaka miwili lakini zilitokea changamoto nyingi ambapo mkataba uliongezwa hadi mwezi Mei 2023 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 71 ya ujenzi na hakuna meli kubwa kama hii kwenye ukanda wa maziwa makuu." Amefafanua Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Erick Hamis
Bwana Hamis ameongeza kuwa Meli hiyo inajengwa na watanzania zaidi 200 na wataalamu kutoka nje wapo 6 tu na ifikapo mwezi wa 10 mwaka huu meli hii itaingizwa kwenye maji ambapo matengenezo mengine yataendelea ikiwa kwenye maji.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.