Kamati ya Fedha na Uongozi Halmashauri ya Jiji la Mwanza leo ta24/05/2024 imefanya ziara kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri ya Jiji hilo.
Akiongoza Kamati hiyo Mhe.Kotecha ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo amewaeleza wajumbe wa kamati na wataalamu kutoka Idara na Vitengo mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, umuhimu wao katika suala zima la kukagua miradi hiyo na kujiridhisha na namna miradi hiyo inavyofanyika hasa kwa kuzingatia umuhimu na upekee wake kwa jamii ya Wilaya ya Nyamagana.
Miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo ni Ujenzi wa Vyumba kumi vya madarasa na vya ofisi nne katika Shule ya Msingi Nyerere iliyoko kata ya Igoma wenye thamani ya Shilingi Milioni 270, Mradi wa ujenzi wa Barabara yenye urefu wa Kilomita 14.4 kutoka Buhongwa hadi Igoma wenye thamani ya Shilingi Bilioni 22.3 ulioanza Machi 2024 na unatarajiwa kukamilika Februari 2025.
Aidha Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa bweni kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Buhongwa ulioanza Mwaka 2021 na unatarajiwa kukamilika June 2024, Mradi wa ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa vyenye thamani ya Shilingi Milioni 100 ulioanza Mei 2024 na unatarajiwa kukamilika June 17, 2024. Pia Mradi wa ujenzi wa Soko kuu la kisasa lenye thamani ya Shilingi Bilioni 23 amabao kwa sasa umefikia asilimia 94 kukamilika.
Akizungumzia mradi wa Barabara ya Buhongwa-Igoma Mhe.Donata Gapi Diwani wa Kata ya Mkuyuni amemtaka Mkandarasi wa ujenzi wa Barabara hiyo Eng.Yusuph Kalemani kuihakikishia Kamati hiyo juu ya ukomo wa mradi huo kwani hadi sasa imebaki miezi tisa tu kati ya miezi 18 aliyopewa Mkataba wake Kufika mwisho na mradi uko hatua za awali.
Kadhalika Mhe.Donata amehoji juu ya suala la wananchi wakazi wanaopitiwa na mradi huo kutopata ajira na badala yake ajira hizo kutolewa kwa watu wasio wenyeji.
Akijibu hoja hizo Eng.Yusuph amesema kuwa changamoto kubwa ya kutoanza mradi huo kwa wakati ni kuchelewa kufika kwa vitendea kazi muhimu katika eneo la kazi na kuahidi kuwa mara baada ya vifaa hivyo kufika Kampuni imejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Aidha kuhusu suala la ajira kwa Wananchi walio katika eneo la mradi, Eng. Yusuph amesema kuwa utaratibu wa kupata ajira mahali hapo ni kutuma maombi na kwamba ajira hizo hutoka kwa wageni tu si rahisi kugundua.
Mwisho, Mhe. Kotecha amewashukuru wajumbe na Wataalamu wote walioshiriki katika ukaguzi huo wa miradi na kusisitiza kila Diwani ambaye mradi upo katika eneo lake ajitahidi kufuatilia utekelezaji wake ili miradi yote ikamilike kwa wakati.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.