Kaimu Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa OR - TAMISEMI Ndg.Stephen Motambi ameitaka Jumuiya ya LVRLAC kuendelea kuisaidia Serikali katika kuhimiza matumizi sahihi ya Ziwa Victoria Pamoja na maeneo ya Nchi kavu ili kupunguza athari za mabadiliko ya Tabia Nchi na Upotevu wa Viumbe maji.
Kaimu huyo ambaye pia ni Mgeni rasmi, amezunguza hayo katika Mkutano wa Wadau wa Maendelelo uliofanyika Aprili 04, 2024 Jijini Mwanza ukidhaminiwa na Benki ya NMB, na kuhudhuriwa na Mameya/Wenyeviti, Wakurugenzi, Madiwani, wataalamu na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka Halmashauri wanachama wa Jumuiya hiyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Kanda ya Ziwa Victoria.
Aliongeza kuwa “uwepo wa Jumuiya hizi unasaidia katika utendaji wa kazi zetu kwa sababu TAMISEMI haifanyi kazi peke yake bali kwa ushirikiano na Jumuiya hizi Pamoja na Taasisi za serikali na binafsi. Hivyo ni vyema kwa wanachama kuunganisha nguvu kwa Pamoja kutekeleza miradi ya mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya Tabia Nchi Pamoja na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla”.
“Lakini pia Wanachama Mlipe michango ya Ada za uanachama ili kuiwezesha Jumuiya kufanya kazi yake Vizuri” aliongeza Ndg.Stephen Motambi Kaimu Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mhe.William Patrick Gumbo ameeleza kuwa kumekuwa na uchafuzi mkubwa ndani ya Ziwa Victoria ambao umesababisha athari kubwa katika suala la uvuvi na kupelekea kuwepo kwa uhaba wa Samaki ndani ya Ziwa hilo, hivyo kupelekea kuwepo kwa uhaba wa kitoweo na kuchangia baadhi ya viwanda vya Samaki kufungwa hususani katika Manispaa ya Musoma.
Pia ameeleza kuwa sababu za kupungua kwa samaki ni pamoja na shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika kingo za Ziwa Victoria kama vile ukataji miti, utupaji hovyo wa taka ngumu zenye sumu zinazo ingia ndani ya ziwa, mifuko na chupa za plastiki zisizooza kwa haraka na hivyo kama Jumuiya tumeazimia kila Halmashauri kupitia vyombo vya ulinzi wa Ziwa BMU kuhakikisha Ziwa linalindwa na watu wazingatie sheria, kanuni na taratibu za uvuvi.
Kwa upande wake Ndg. Billy Brown ambaye ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya LVRLAC Kanda ya Tanzania ameongeza kwa kusema “Hamasisho la Jumuiya ni kwamba Halmashauri zote zinazozunguka Ziwa Victoria ziendelee kutumia nafasi yake kama Halmashauri kupitia wataalamu wake wa uvuvi kuendelea kufuatilia sheria na kanuni mbalimbali zilizowekwa na mamlaka zinazohusiana na utunzaji wa mazingira na za uvuvi ili wavuvi waendelee kulinda mazao ya uvuvi yanayo patikana ndani ya ziwa Victoria”.
Vilevile, amesema kuwa uvuvi mbadala wa kufuga Samaki kwa njia ya vizimba unaohamasishwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan uzingatiwe na Vijana wetu wapewe elimu Zaidi ili watu waache uvuvi haramu jambo litakalotupatia fursa ya kupata Samaki si kwa kitoweo tu bali pia kutoa ajira kwa Vijana na akina mama na kwa kutupatia kipato.
Nao wadau mbalimbali wa maendeleo walioshiriki Mkutano huo wamechangia mawazo yao juu ya uendelezaji na utunzaji wa rasilmali Ziwa Victoria, kwa kuanza naye Ndg.Hemed Aziz Mtaalamu wa Ushirika kati ya Serikali na Taasisi Binafsi (Public Private Partnership) amehimiza Halmashauri wanachama wa Jumuiya hiyo kutumia mfumo wa PPP katika kusuluhisha changamoto za maendeleo hususani mazingira.
Kadhalika, Mratibu wa Mradi wa Fukwe za Maziwa Makuu (GreatLakes Clean Shores) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameomba umoja huu kuhakikisha unalinda Ziwa Victoria dhidi ya taka za plastiki ambazo chembechembe zake huingia mpaka tumboni mwa Samaki na baadae kuleta madhara kwa binadamu.
Aliongeza kuwa Halmashauri hizo zishirikiane na watu wenye ujuzi na tekinolojia wezeshi katika kuchakata taka za plastiki na kufanya urejeshi ili kuweza kutumika kwa namna nyingine. Hivyo badala ya kutupwa ovyo iwe ni fursa ya kujitengenezea kipato kwa Halmashauri na jamii kwa ujumla.
Vilevile Mtaalamu wa Mazingira Ndg.Fanuel Kasenene Kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza amewakumbusha wanachama wa Jumuiya kusimamia vyema fukwe zao na kuziendeleza kwa kubuni miradi Rafiki itakayo tekelezwa katika fukwe hizo ili kuongeza kipato kwa Halamashauri kama wamiliki na wananchi kwa ujumla na hivyo kukamilisha maana ya uchumi wa bluu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Nishati Mbadala (Chabri Energy) Ndg.Bernard Makachia amesema “ukitazama kauli mbiu ya Mkutano huu inasema kuhamasisha juhudi unganifu kati ya wadau wa Ziwa Victoria ili kuibua suluhishi bunifu kwa changamoto za mazingira, sehemu ambayo mimi naingia moja kwa moja kutokana na kuwa mtengenezaji wa majiko na kuni mbadala ambazo huzalisha nishati safi ya kupikia”.
“Nishati hii ni safi na inatumika sehemu zote, hivyo niwasihi wajumbe wa mkutano kutumia nishati hii mbadala ili kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kampeni yake ya ‘Clean Cooking’ ambayo itasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia Nchi”. Aliongeza Ndg. Bernard Makachia
Wakihitimisha kikao hicho wajumbe waliazimia kulitunza vyema Ziwa Victoria kwa kudhibiti utupaji hovyo wa taka ngumu Pamoja na kutumia nishati mbadala katika shughuli za kila siku za kibinadamu ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Wajumbe wa Mkutano wa Wadau wa Maendeleo wakielekea kuzuru vizimba vya kufugia samaki vilivyotolewa na Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.