Halmashauri ya Jiji la Mwanza imezindua ugawaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa makundi maalumu yakiwemo ya wanawake,vijana na walemavu ambapo takribani Bilioni 1.3 imetolewa kwa vikundi vyenye sifa.
Akifungua uzinduzi huo leo Februari 20, 2025 katika uwanja wa Nyamagana Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe, Amina Makilagi amempongeza Mhe Rais Dr Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo ya asilimia 10% isiyokuwa na riba ambapo itavinufaisha vikundi 87 vilivyokidhi vigezo na kupata sifa ya kupata mkopo kwa lengo la kuanzisha biashara mbalimbali ili kujiinua kiuchumi.
Aidha Makilagi ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia Mkurugenzi, Meya na Madiwaji kwa usimamizi mzuri wa mapato huku akisema asilimia 70% ya mapato inaenda kwenye Miradi, asilimia 10% inaenda kwenye mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu na kuongeza kuwa hadi sasa wametenga Bilioni 3.8 ambapo leo wametoa Bilioni 1.3 na zimebaki 2.5 ambazo zitatolewa kwa wanufaika wa awamu ya tatu kwa watakaokidhi vigezo baada ya kufanyiwa upembuzi yakinifu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mhe. Stanslaus Mabula amewapongeza wanufaika wa mkopo wa asilimia 10% na kuwataka warejeshe marejesho yao kwa wakati,huku akisema fedha bado zipo na kwamba Halmashauri inatarajia kutoa hadi Bilioni 5 na kuongeza kuwa vikundi vitakavyorejesha kwa wakati vitapewa mkopo mpya huku akisema hana shaka na vukundi vyote kwa kuwa kamati ilijiridhisha kuwa vikundi vyote ni hai kabla ya kutoa mkopo.
Aidha Meya wa Jiji, Mhe. Sima Constantine amewataka wanufaika wakawe mabalozi wazuri kwa kuwa walipewa elimu ya namna ya kutumia fedha hizo za asilimia 10% zisizokuwa na riba na pia kuunga mkono suala zima la utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi yakupikia.
Vilevile Bi zena Kapama , ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Maendeleo ya Jamii amesema Mikopo hii ya asimia 10% wanapewa wanaoanzisha mitaji na wale wanaoendeleza mitaji kwa wenye umri wa miaka 18-45 na mikopo haina riba lakini pia amewataka katika biashara watakazozifanya walipe ushuru ili kuendeleza kutunisha mfuko wa Wanawake, Vijana na walemavu.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.