Hospitali ya Nyamagana yakabidhiwa gari jipya la wagonjwa (Ambulance) lenye namba ya usajili STM 7781 ambalo litasaidia kupeleka huduma karibu pamoja na kuokoa maisha ya wananchi wa Jiji la Mwanza.
Mgeni Rasmi katika Hafla hiyo Mhe.Stanslausi Mabula Mbunge wa Nyamagana, amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa katika kuwaletea maendeleo watanzania.
Aidha, ameieleza hadhara kuwa Nyamagana inatakiwa iwe na hospitali yenye hadhi na sifa ya kuwa Hospitali ya Wilaya, hivyo ili kupunguza mzigo wa hospitali hiyo serikali itakwenda kufungua vituo vya afya maeneo tofauti tofauti ya Wilaya,kwa kuwa uongozi huu wa awamu ya sita unajali na kuthamini maslahi ya wananchi na wafanyakazi.
Vilevile ameongeza kuwa serikali imeleta fedha zaidi ya Billioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa tatu ili kupunguza msongamano wa wagonjwa pindi wanapokuja kutibiwa hospitalini hapo lakini pia hospitali hiyo itapokea gari la utawala siku za hivi karibuni.
Naye Mganga mkuu wa Hospitali ya Nyamagana Dkt.Sebastian Pima ameieleza hadhara kuwa kuletewa gari jipya la wagonjwa kutasaidia kupeleka huduma karibu na wanachi suala litakalosaidia kuokoa maisha ya wana Nyamagana.
“kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali tumeweza kujenga kituo cha afya Bulale na pia tumepandisha hadhi zahanati ya Mkolani, Mandu, na Fumagira kuwa vituo vya afya, vilevile tunampango wa kujenga hospitali ya Nyegezi ili kuipunguzia mzigo hospitali ya Nyamagana” aliongeza Dkt.Pima.
Dkt. Pima pia ameungana na Mbunge kuishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha Tshs millioni 800, ambapo mpaka sasa kwenye akaunti ya hospitali hiyo kuna zaidi ya Tshs Billioni 1 ambayo itakatumika kujenga jengo la ghorofa tatu litakalokuwa na huduma za mionzi, kliniki za kibingwa na wodi za kulaza wagonjwa kwani kila mwaka zaidi ya wanawake 650 hadi 700 hujifungua hospitalini hapo, hivyo jengo hilo litasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa.
Aidha Diwani wa Butimba Mhe, Marwa Mbusilo. Ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuipatia hospitali ya Nyamagana gari la wagonjwa (Ambulance) kwani itasaidia pindi watu wanapopewa rufaa kwenda hospitali ya kanda au ya rufaa kusafirishwa kwa haraka.
Vilevile, Mwenyekiti wa mtaa wa Butimba Ndg.Faustin Mtonja amempongeza Mbunge wa Nyamaga kwa kuendelea kulitetea Jimbo lake kwani bila yeye kuisemea miradi wasingeweza kupata chochote. Pia amewapongeza viongozi wote wa serikali kwa jitihada wanazozifanya katika kuikuza hospitali hiyo kwani inahudumia pia watu kutoka nje ya Nyamagana.
Hafla hiyo imehitimishwa kwa tukio la Mbunge wa Nyamagana kukabidhi gari la hilo la wagonjwa lenye vitu vya msingi ndani yake na vinavyotumika kwa dharula kama vile radio call, sehemu ya mtungi wa dharula, sehemu ya kuchaji, kabati, na kitanda. Hivyo kawaasa kuwa gari hilo litumike wakati wa dharula tu ili kuokoa maisha ya wananchi na sio vinginevyo.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.