Stendi kuu ya mabasi Nyegezi imekuwa mfano bora wa usimamizi wa miundombinu ya usafiri wa umma, na hivyo kuvutia viongozi kutoka Halmashauri nyingine kutembelea na kujifunza pamoja na kubadilishana uzoefu, kuiga mbinu bora na kujenga ushirikiano wa kikazi baina ya halmashauri.
Juni 10,2025 Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imefanya ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa lengo la kujifunza mbinu bora za kuongeza mapato, hasa kupitia usimamizi wa stendi kuu ya mabasi Nyegezi.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati waliambatana na Waheshimiwa Madiwani, Wataalamu pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali kutoka Hanang. Wakiwa Jijini Mwanza, wametembelea stendi kuu ya mabasi ya Nyegezi ambapo walijionea kwa vitendo namna ya uendeshaji wa stendi hiyo na jinsi teknolojia ya kisasa inavyotumika katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake Meneja wa Stendi kuu ya mabasi Nyegezi Bw. Fredrick Machugu waliwasilisha taarifa juu ya mikakati inayotumika kuboresha mapato, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa mifumo ya kidigitali na uwazi katika ukusanyaji na ushirikishwaji wa wadau wote katika sekta ya usafiri wa abiria.
Aidha ziara hiyo imetoa fursa kwa viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Hanang kuona kwa macho yao mifumo inayofanya kazi kwa ufanisi na kuelewa jinsi wanavyoweza kuitafsiri na kuitumia kwenye halmashauri yao. Pia imesaidia kuimarisha mahusiano kati ya halmashauri hizi mbili kwa lengo la kuendeleza ushirikiano wa kitaalamu na kimaendeleo.
Kupitia ziara hii ya kimafunzo, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imepata maarifa muhimu ya kuboresha mbinu za ukusanyaji mapato kupitia usimamizi bora wa stendi za mabasi. Uzoefu walioupata Mwanza utasaidia kuleta mabadiliko chanya katika mifumo ya mapato ya Hanang, hatimaye kuinua huduma kwa wananchi na kukuza maendeleo ya halmashauri yao.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.