Afisa Elimu Taaluma wa Jiji la Mwanza, Bw. Julius Magembe, leo tarehe 26 Juni, 2025, amefungua rasmi kikao kazi cha Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii uliopo Stendi Kuu Nyegezi, na kimejikita katika kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na watoto na vijana wa mtaani na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji Wakili Kiomoni Kibamba, Bw. Magembe aliwapongeza Maafisa Ustawi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwalinda watoto na vijana, na kuwataka waendelee kutoa huduma zenye huruma na weledi kwa makundi hayo maalum katika jamii.
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Bi. Anitha Joseph, Afisa Mradi kutoka Shirika la Railway Children Africa, ameeleza kuwa mradi huo wa miaka miwili unalenga kusaidia watoto wenye umri wa miaka 8–14 na vijana wa miaka 14–18 wanaoishi au wanaofanya kazi mitaani na kusisitiza kuwa lengo la shirika hilo ni kutengeneza mabadiliko chanya ya muda mrefu kwa watoto na vijana hao.
“Lengo letu ni kuona jamii salama kwa watoto na vijana, huku tukihamasisha jamii kuwajibika katika kuzuia watoto kuingia mitaani na katika mazingira hatarishi,” alisema Bi. Anitha.
Aidha, amebainisha kuwa Shirika hilo lina mpango wa kufanya kazi na serikali katika kutengeneza miongozo na sheria maalum za kuwalinda watoto hao na kuhakikisha ulinzi wa kijamii unafikiwa kwa vitendo.
“Tutafanya mazungumzo na serikali ili kutengeneza miongozo na sheria ambazo zitawalinda watoto na vijana walio katika mazingira hatarishi” Amesema Afisa Mradi.
Anitha ameongeza kuwa Railway Children Africa pia linaendesha “Mradi Mama”, unaolenga kuzuia watoto wasitoke majumbani na kuingia mitaani kupitia ushirikiano na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata na Watendaji wa Mitaa na wazazi wanaobainika kuwa watoto wao wako kwenye hatari ya kuingia mitaani hupewa mafunzo ya malezi bora na kupewa msaada wa kijamii.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jiji la Mwanza, Bi. Edith Ngowi, ameeleza kuwa kuna madawati 14 ya kitaifa yanayotekeleza mwongozo maalum unaobainisha majukumu ya kila mdau katika Halmashauri, Idara ya Elimu, na Mipango Miji katika kulinda watoto na vijana walioko katika mazingira magumu.
Bi. Edith Nkiwa, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Nyamagana, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu wamefanikiwa kuwaokoa watoto na vijana 309 waliokuwa wakikumbwa na ukatili wa aina mbalimbali na kusisitiza kuwa mazingira wanayofanyia kazi kwa sasa ni wazi, yanayowezesha kutokomeza ukatili kwa ufanisi.
Bw. Magembe amewasisitiza Maafisa Ustawi kuhakikisha kuwa watoto wanaoishi mitaani wanarudishwa kwao, na jamii inapatiwa elimu ya kutosha juu ya madhara yanayowakumba watoto hao, ili kuzuia ongezeko la tatizo hilo.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.