Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Nassoro Makilagi na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya, amewaongoza wajumbe kutoa ushauri katika Kikao cha mapendekezo ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mhe. Mkuu wa wilaya ya Nyamagana ameweeleza wajumbe umuhimu wa bajeti hii kwani ni kwa ajili ya maendeleo ya wilaya ya Nyamagana na Jiji la Mwanza kwa ujumla. Hivyo aliwakaribisha wajumbe kutoa ushauri juu ya bajeti iliyopendekezwa kwa mwaka 2024/25.
Ambapo, Mjumbe Charles Paulo Kisamba, alishauri kutenga bajeti kwa ajili ya maboresho ya Uwanja wa mpira wa Nyamagana kwa kujenga majukwaa lakini pia kuipandisha hadhi timu ya Pamba Jiji FC ili kuweza kukuza uchumi wa Jiji la Mwanza pindi ligi zipochezwa.
Vilevile, Mwenyekiti wa Soko la Mabatini Ndg.Zuwena Muhamudu ametoa pongezi kwa bajeti iliyotengwa kwa ajili ya masoko na kupendekeza maeneo ya mama lishe yajengwe kwa mfumo utakao ruhusu majiko ya gesi ilikuondoa matumizi ya mkaa.
Ameongeza kuwa ni muhimu kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha daraja la Mkuyuni ili kuepuka adha ya kuhudumia wananchi wa upande mmoja na wakati mwingine kupoteza mawasiliano kati ya upande mmoja na mwingine, pindi yatokeapo majanga ya mvua.
Naye Mwenyekiti wa Chadema Ndg. Charles ameshauri kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo zitumike kama zilivyopangwa na sio vinginevyo. Pia aliongeza kuwa wajumbe wapewe makabrasha mapema kabla ya siku ya kikao ili waweze kuipitia vizuri taarifa itakayo jadiliwa kwenye kikao husika.
Kufuatia majadiliano hayo, Mwenyekiti wa Kikao Mhe. Amina Makilagi amepokea maoni na ushauri wa wajumbe juu ya mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2024/2025 na kuahidi kuyafanyia kazi kwani bajeti hii ni kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Nyamagana.
Ameongeza kuwa atatembelea miradi ya maendeleo ili kujiridhisha kama fedha za bajeti zinafanya kazi kama ilivyopangwa.
Baada ya majadiliano hayo wajumbe walipitisha mapendekezo ya Bajeti ya Mwaka 2024/25, hivyo Mwenyekiti alimkabidhi Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Mhe.Sima Constantine Sima kwa ajili ya kuichakata tena katika baraza la madiwani na baadae kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa kwa hatua zingine.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.