Katika kuhakikisha jamii inashirikiana na Serikali katika kuchangia maendeleo ya kijamii, kisiasa na inasaidia kuweka msingi wa utawala bora na maendeleo endelevu, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ameendesha mikutano ya hadhara katika kata ya Mbugani na Mkolani.
Katika mikutano hiyo iliyofanyika Machi 27 na 28, 2025, wananchi wa mtaa wa Mzambalauni, Nyamazobe na Ibanda wamepata nafasi ya kutoa kero zao ampapo miongoni mwa kero zilizotajwa ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, umeme, maji na upungufu wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya Shule.
Kwa upande wa changamoto ya maji walisema, ”Maji yanatoka mara moja kwa wiki au muda mwingine hata hiyo wiki yanaweza yasitoke tunalazimika kununua maji kwa gharama kubwa kutoka katika maeneo jirani jambo ambalo kwa baadhi ya watu imekuwa ni ngumu kumudu gharama za ununuzi wa maji” walisema.
Akizungumza na wananchi hao Mhe. Makilagi alisema Serikali imetoa bilioni 46 kwa ajili ya kujenga matenki katika mitaa minne na kusambaza mabomba.
"Mtaa wa Nyamazobe litajengwa tenki la lita milioni tano na litasambaza maji katika Mitaa ya Kata ya Mkolani, Sahwa litajengwa la lita milioni 10, Buhongwa Lita milioni 10 na Fumagila lita milioni 10" alisema Makilagi.
Alisema katika ujenzi wa matenki hayo umeshaanza kutekelezwa katika mitaa miwili ambayo ni Buhongwa na Sahwa.
"Nyamazobe na Fumagila ujenzi haujaanza kutokana na wananchi waliopitiwa na ujenzi wa mradi huo kusubiri fidia zao" alisema Makilagi na kuongeza ,
"Tenki hili linalojengwa katika Mtaa wenu wa Nyamazobe na litakuwa suluhisho la kero ya maji safi na salama inayowakabili" alisema Makilagi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usambazaji Maji kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA), Bw. Celestine Mahubi alisema wananchi waliopitiwa na mradi huo ni 36 hivyo wanasubiRi walipwe fidia ili mkandarasi aanze kazi.
Aidha katika kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa Mhe. Makilagi alitoa maelekezo kwa wataalam alioambatana nao kuhakikisha wanashughulikia changamoto zote zilizotajwa na wananchi ili kuboresha huduma stahiki kwa wakati.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.