Uzinduzi wa kamati ya ushauri wa kisheria ya Wilaya na uzinduzi wa Kilniki ya sheria ya bure kwa wananchi wa Nyamagana imezinduliwa Machi 25, 2025 katika uwanja wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana-Mkolani kwa lengo la kuwataka wananchi wote wanaohitaji msaada wa kisheria ndani ya Nyamagana kuhudumiwa bure.
Akizindua kamati hiyo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema kamati ya ushauri wa kisheria kwa ngazi ya Mikoa na wilaya zimeanzishwa kwa mujibu wa mwongozo wa huduma za kisheria katika Mkoa na wilaya kwa sheria ya mwaka 2024 huku zikilenga kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi, watumishi wa Umma na Viongozi wa Umma ili kutatua changamoto za kisheria zinazojitokeza katika Jamii zetu.
Akizungumza na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika uzinduzi huo kwa kutoa faida za kuanzishwa kwa msaada wa kisheria katika wilaya ikiwa ni kupunguza migogoro dhidi ya Serikali, kukutanisha Mawakili wa serikali na taasisi mbalimbali na kusaidia wananchi kutatua changamoto zao, kupunguza malalamiko ya kisheria kutoka kwa wananchi pamoja na kupunguza vitendo vya uonevu na vinavyovunja sheria na taratibu kwa ujumla.
Aidha Mhe. Makilagi ameeleza kuwa uzinduzi wa kamati ya huduma ya kisheria utasaidia kutoa elimu kwa viongozi ili watakapokuwa wanahudumia wananchi watende haki huku akiahidi kutoa ushirikiano kwani jukumu la serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa kamati ili watimize wajibu wao na kuleta matokeo chanya yanayokusudiwa na Wananchi.
Neila Chamba ambae ni Mwenyekiti wa kamati ya Sheria Wilaya ya Nyamagana, ametoa salam za kamati na kuahidi kutoa ushirikiano katika ofisi ya Mkuu wa wilaya na kushirikiana na wadau mbalimbali kuweza kutatua changamoto za kisheria kulingana na miongozo inavyowataka kutekeleza majukumu yao kisheria.
Naye Nuru Lusekero, wakili wa serikali ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuunda kamati ya ushauri wa kisheria huku akieleza kamati hii imeudwa kwa kutumia mwongozo uliotolewa na Mwanasheria mkuu wa serikali hivyo kamati hizi zinafanya kazi kwa niaba ya mwanasheria mkuu wa serikali.
Vilevile zinatakiwa kufanya kazi na maafsa wa idara mbalimbali kulingana na kesi husika ikiwa ni utekelezaji wa malengo ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yakwamba kila Taasisi ya serikali kusikiliza malalamiko ya wananchi wakati wote ili kupunguza mashauri dhidi ya Serikali.
Kutokana na migogoro mingi katika jamii Mhe. Makilagi ametoa maelekezo kwa kamati kuzingatia yafuatayo; Kuendelea kuboresha kiwango cha utoaji wa huduma ya kisheria na kuongeza wigo katika maeneo ambayo hayajafikiwa hasa maeneo ya pembezoni mwa mji, kushirikisha watu mbalimbali ili kuboresha huduma na kujiwekea utaratibu kisheria wa kuandaa kilniki kwa kuwafata wananchi katika maeneo yao .
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.