Katika kuendeleza juhudi za maendeleo ya jamii, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi wa miradi mbalimbali ya kijamii.
Akizungumza na wenyeviti wa mitaa na watendaji wa Kata na Mitaa katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi mkubwa wa Jiji June 2, 2025 amesema ushiriki wa wananchi si tu kwamba unaongeza uwazi na uwajibikaji, bali pia unajenga umiliki wa miradi hiyo na kuhakikisha utekelezaji wake unaleta tija kwa jamii nzima.
Akizungumza katika kikao cha maandalizi ya uzinduzi wa miradi hiyo, DC alisema kuwa serikali imekuwa ikiwekeza rasilimali nyingi katika miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu, hivyo ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu siyo tu kwenye uzinduzi, bali pia katika ufuatiliaji wa utekelezaji.
"Miradi hii ni kwa manufaa ya wananchi wote. Tukiwa na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wananchi, tutahakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vya juu na ndani ya muda uliopangwa," alieleza DC.
Aidha, alisisitiza kuwa uzinduzi wa miradi ni sehemu ya uwazi wa serikali katika kuonesha matumizi ya fedha za umma na mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuutaja mradi wa Maji Butimba kuwa ndio utakaozinduliwa.
Kwa upande wao, Wenyeviti na watendaji walioshiriki katika kikao hicho walieleza kufurahishwa na hatua ya serikali kuwashirikisha wananchi moja kwa moja, wakiahidi kwenda kutoa Elimu juu ya umuhimu wa kushiriki katika zoezi la uzinduzi wa miradi na kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.