Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Ndg. Thomas James Salala kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Nassoro Makilagi ameongoza kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza tarehe 14/02/2024 chenye lengo la kujadili namna ya kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii juu ya chanjo ya Surua Rubella.
Kufuatia kikao hicho, Mratibu wa chanjo, Ndugu Makubi Masaga Gondera amewaeleza wajumbe kuwa Chanjo ya ugonjwa wa Surua Rubella itaanza kutolewa tarehe 15-18 Februari,2024 na kampeni itafanyika ndani ya siku 4 ambapo watoto takribani 81,449 watachanjwa na jumla ya dozi 85,520 za chanjo za Surua Rubella zimepokelewa katika wilaya ya Nyamagana na zikusambazwa katika vituo maalum vya kutolea chanjo, wahusika wa chanjo hii ni watoto kuanzia miezi 9 hadi miaka 4 na miezi 11 bila kujali chanjo walokwisha kupewa mwanzo kwa kuwa haina madhara bali inaongeza nguvu na kumfanya mtoto awe na kinga imara.
Ndg, Makubi Masaga Gondera ameongeza kuwa kampeini hii yenye kaulimbiu '' Onyesha upendo, Mpeleke Mtoto akapate chanjo'' inawataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto katika vituo vya huduma ya chanjo ili kupata chanjo hiyo kikamilifu ambapo mtoto atachomwa akiwa na miezi 9 na kuirudia baada ya miezi 18, hii inafanyika kumkinga mtoto dhidi ya viusi vya "Morbilli virus paramyxrus" vinavyosababisha ugonjwa huo.
Naye Mwenyekiti wa wenyeviti wa mitaa wa mtaa wa Bugando Jiji la Mwanza, Ndg Juma R. Masanja. Ameshauri wajumbe wa kamati hiyo kuwekeza nguvu kubwa kwa viongozi wa ngazi ya chini ili kuhakikisha elimu ya kampeni ya chanjo inawafikia wananchi wote na kutowa wito kwa serikali kuwawezesha mahali penye uhitaji ili kusambaza taarifa kwa haraka.
Kwa upande wake Ndg, Juma Yusuphu Mwakilishi wa Shekhe wa Wilaya ametoa maoni yake nakusema "Jamii zetu bado zinawasiwasi na chanjo zinazotolewa kwa sababu watu hawana uelewa nazo hivyo ni vyema kushiriki kikamilifu katika kampeni ya chanjo kwa kuwaelimisha wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa chanjo itakayotolewa kwa Watoto.
Akihitimisha kikao hicho Ndg, Thomas James Salala amesisitiza kuwa ujumbe sahihi utolewe kwa jamii juu ya chanjo hii na kutoa onyo kwa wale wote watakao potosha na kukwamisha zoezi hili na kwamba taarifa za upotoshaji zitolewe sehemu husika.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.