Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Mhe, Sima C. Sima ameongoza kikao cha Madiwani na wajumbe kujadili mapendelezo ya mpango wa bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa Mwaka wa fedha 2024/2025.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Mhe, Sima amewataka madiwani na wajumbe kutoa mapendekezo, ushauri na maoni yenye tija katika bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwani bajeti ndiyo kila kitu kwenye Halmashauri na hivyo kutazama kwa umakini miradi iliyoainiswa kama inatija kwa Jiji letu la Mwanza.
Mbunge wa Nyamagana Mhe, Stansilaus Mabula, amesisitiza kuwa soko la makoroboi lijengwe kawaida na siyo ghorofa kwa kuzingatia uchumi wa wafanyabiashara wenyewe. Pia alishauri kupunguza kiasi cha fedha kwa baadhi ya maeneo ili zitumike kurekebisha miundombinu.
Aliongeza kuwa maeneo yanayolegalega yafanyiwe kazi kwani mpaka sasa kati ya miradi 36 iliyotekelezwa ni miwili tu ilihali tunafahamu miradi ndiyo inayoleta uhai kwenye Halmashauri zetu.
Naye Mhe.Diwani Dionis Salala kupitia bajeti hii ameiomba Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha wanalipa fidia wanachi kwa ajili ya kuchukua mashamba ya mradi wa upimaji viwanja na kushauri kupeleka miundombinu maeneo husika ili iwe rahisi kwa wadau kuvutiwa na maeneo hayo.
Pia, Mhe.Diwan Edith ameshauri kuwa kipaumbele cha shule ya msingi Nyaborogoya kiwe ni matundu ya vyoo na siyo madawati, kwani changamoto kubwa sana katika shule hiyo ni vyoo.
Katibu Mwenezi Ccm wilaya Mhe. Mustapha Banigwa amesema kuwa kutokana na kutokuwepo kwa chanzo kipya cha mapato ni vyema wataalamu watoke nje wakajifunze mbinu za kubuni miradi mipya itakayokuza pato la Mwanza. pia ameshauri kuwa daraja linalounganisha Mkolani na Nyegezi likarabatiwe haraka ili kuendelea kuwepo mawasiliano mazuri baina ya pande zote mbili.
Mwisho Mwenyekiti wa Baraza la madiwani Mhe. Sima amemwambia Mkurugenzi kupitia timu yake ya wataalamu kuchakata mapendekezo yanayofaa nakuyafanyia kazi kwa masilahi ya Jiji la mwanza na kuwaomba watumishi wanaolegalega katika utendaji kazi kujitathimini na kufanya kazi kwa kujitoa huku wakibuni mbinu za kuweza kuliongezea Jiji la Mwanza mapato mengi kwa kuzalisha fursa ambazo ni vipaumbele kwa wananchi.
Mara baada ya majadiliano hayo baraza lilipitisha Bajeti hiyo itakayotumika mwaka wa fedha 2024/2025.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.