Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Mwanza limeridhia kupitisha rasimu ya bajeti ya Shilingi bilioni 124,378,085,328.00 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kikao hicho kimeketi katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Februari 21,2025 na kuongozwa na Mwenyekiti Mhe. Bhiku Kotecha ambaye ni Naibu Meya.
Katika kikao hicho Mwenyekiti Mhe Bhiku Kotecha, amesema Bajeti iliyojadiliwa na Madiwani na kupitiswa kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imezingatia utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (Ccm) ya Mwaka 2020 na miongozo mingine ya kitaifa.
Aidha amemtaka Mkurugenzi na timu yake kuendelea kujituma katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kutekeleza miradi ya maendeleo na kuyafanyia kazi yote yaliyojadiliwa na Waheshimiwa Madiwani ili kuijenga Nyamagana kwa kuwaletea Wananchi maendeleo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Mhe. Amina Nassor Makilagi kwa niaba ya kamati hiyo amewapongeza waheshimiwa Madiwani kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato na miradi ya Maendeleo inayotekelezwa kwa mapato ya ndani katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Pia Mkuu wa idara ya Uchumi Bw. Jeremiah Lubereje amevitaja vipaumbele vilivyopangwa kutekelezwa na Halmashauri kupitia bajeti ya mwaka 2025/2026 kuwa ni kuboresha Miundombinu ya Barabara kwa kutenga asilimia 10%, Elimu, Afya, kujenga miundombinu ya kisasa ya Maduka, parking za magari Mjini kati, kutenga asilimia 10% ya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu, kuimarisha sanaa na michezo, kujenga masoko mawili mapya na kuboresha mengine mawili kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiasha kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki.
Vilevile Diwani wa viti Maalum kutoka kata ya Kishiri Mhe.Magreth Paul amewataka TARURA Kuhakikisha wanazifanyia kazi Barabara za kishiri kwa kuwa ina wakazi wengi na inaunganisha kata jirani ya kisesa hivyo amemtaka kaimu Meneja Christopher Mgamba kulifanyia kazi suala hilo kwa kutenga bajeti ya matengenezo ya Barabara za kishiri huku akisema zimesahaurika.
Naibu Meya na Mwenyekiti wa kikao cha Baraza Mhe. Bhiku Kotecha amemuagiza Mkurugenzi na timu yake kuyafanyia kazi maelekezo ya waheshimiwa Madiwani ili kuhakikisha kuwa bajeti iliyopitishwa inaleta maendeleo katika jamii ndani ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.