Ziara za viongozi zimeendelea kuwa na mchango mkubwa kwa wananchi, kwani zinatoa fursa ya kipekee kwa wananchi kukutana ana kwa ana na viongozi wao, kueleza changamoto, kero na mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya jamii zao. Kupitia mikutano ya hadhara, wananchi husikilizwa na kupata mrejesho wa moja kwa moja juu ya masuala yanayowagusa katika maisha yao ya kila siku.
Akizungumza leo katika kikao kilichowakutanisha Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Watendaji wa Kata, kilichofanyika katika Ukumbi wa Gandhi Hall, Makao Makuu ya Wilaya ya Nyamagana, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi, amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kushiriki kikamilifu katika mikutano ya hadhara na kuhakikisha mikutano hiyo inafanyika mara kwa mara katika mitaa yao.
Mhe. Makilagi ameeleza kuwa mikutano hiyo inalenga kuwaelimisha wananchi juu ya masuala ya kiusalama katika maeneo yao, kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na viongozi, pamoja na kutoa nafasi ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataarifu viongozi hao juu ya ujio wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Mwanza, hususan ndani ya Wilaya ya Nyamagana, ambapo lengo kuu la ziara hiyo ni kuzungumza na wananchi kuhusu suala la usalama nchini na kuhimiza ushiriki wa wananchi katika kulinda amani ya Taifa.
Kwa ujumla, wananchi wametakiwa kuendelea kudumisha amani, mshikamano na umoja tulionao kama Taifa, sambamba na kushirikiana na viongozi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.