Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa ili kuwawezesha kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na miongozo ya kazi.
Kwa upande wake Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Leonard Majuto amesema kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa utoaji Elimu kwa watendaji ambayo yatawasaidia kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma huku wakishirikiana na viongozi wengine wakiwemo Madiwani, wenyeviti Katika kusimamia miradi ya maendeleo ndani ya mitaa yao.
“Tayari tumetoa mafunzo kwa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za Mitaa hivyo tunaamini sasa kwa pamoja wataenda kusimamia shughuli za Serikali, kuibua miradi ya maendeleo na kutatua migogoro ya wananchi” amesema Majuto.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ambao ni mwajiriwa wa ajira mpya Olaf Ndunguru na Christina Buha walisema yatawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi ili kuleta maendeleo kwa wananchi huku watendaji walioko kazini akiwemo Caroline Masanja akisema yamewaongezea ari na nguvu mpya kazini.
Naye Dkt. John Kasubi mkufunzi kutoka chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kampasi ya Shinyanga alisema mafunzo hayo yatawasaidia watendaji kushirikiana na wananchi badala ya kujiona mamwinyi kazini.
Aidha Meneja Rasilimaliwatu Chuo cha Hombolo tawi la Shinyanga Boniphace Michael alisema kuwa wamewafundusha mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi ya TEHAMA na umakini wa kutovujisha siri za ofisi. Lakini pia waliwakumbusha kufanya maandalizi sahihi ya kustaafu ili kuwa na maisha mazuri baada ya utumishi wa umma.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.