Ikiwa ni mwendelezo wa kuifanya Nyamagana kuwa ya kijani, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe Amina Makilagi leo tarehe 14/12/2024 amewaongoza wananchi wa Kata ya Buhongwa Katika zoezi la upandaji miti pembezoni mwa barabara ya Buhongwa-Nyakagwe na Shule ya Msingi Amina Makilagi.
Makilagi amesema takribani miti elfu moja imepandwa ikiwemo miti mia sita ya urembo iliyopandwa pembezoni mwa barabara na miti mia nne ya matunda iliyopandwa shule ya Msingi Amina Makilagi.
Aidha amezitaja faida za upandaji na uhifadhi wa miti kuwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji, kuvuta mvua, kuwa na makazi yenye mandhari bora, husaidia kunyonya na kuhifadhi hewa ukaa inayozalishwa na binadamu kutokana na shughuli zake mbalimbali.
Katika hatua nyingine Makilagi amempongeza Mhe. Rais kwa kuwa mwanamazingira namba moja katika nchi yetu na hii inampa nguvu Mhe Mkuu wa wilaya kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe Rais za kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kwamba atahakikisha kwa mwaka huu anavuka lengo la kupanda miti zaidi ya milioni moja.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mwandamizi Bw. Emmanuel Mgimwa ameeleza dhamira ya kupanda miti ya urembo kuwa ni kuyafanya mandhari ya barabara yawe kivutio kwa wageni na wenyeji wanaotumia barabara hiyo na kuwataka wananchi kuilinda na kuitunza miti hiyo. Vile vile ametoa wito kwa wananchi kutembelea vitalu na kuchukua Miche kwa kuwa inatolewa bila gharama yoyote.
Naye Diwani Kata ya Buhongwa Mhe Kabadi Joseph Benard amemshukuru Mkuu wa wilaya ya Nyamagana na Uongozi wa TFS kwa kuifanya Kata ya Buhongwa kuwa mfano Katika zoezi la upandaji miti na kuahidi kuilinda na kuitunza miti hiyo kwa kushirikiana na wananchi pamoja na Taasisi zilizoko ndani ya kata ya Buhongwa.
Ameongeza kuwa kila mwananchi anao wajibu wa kutambua umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kuleta madhara makubwa katika maeneo yetu na Taifa kwa ujumla.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.