Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Dkt. Phillis Nyimbi amepiga marufuku tabia ya vituo vya pikipiki kulazimisha watu kujiunga na vikundi vyao kwa kuwalazimisha kujiunga na vikundi hivyo kwa gharama kubwa.
Akitoa katazo hilo katika kata ya Kishili, mkuu wa Wilaya ameonya vikundi vyote vya pikipiki maarufu kama bodaboda kuacha tabia ya kutafuta pesa kwa njia zisizo halali na badala yake kufuata kasi ya serikali ya awamu ya tano inayosisitiza watu wote kujituma na kufanya kazi bila kubughudhiwa na mtu ama kikundi chochote cha watu.
Mheshimiwa Nyimbi alitoa katazo hili baada ya kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Lushinge Deus kulalamika mbele ya mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Kishili tarehe 21 Disemba ambapo kijana huyo alisema kikundi cha waendesha bodaboda wa Kishili kimemlazimisha kuchangia shilingi milioni moja ili kujiunga na kituo chao kama mwanachama wa kituo chao.
Alisema "nimepata pikipiki ya mkataba lakini baada ya kulipa mkataba na kubakiza shilingi laki saba,nilikwenda kijiwe cha Kishili ili niendelee na shughuli ya kuendesha pikipiki lakini chakushangaza nilipofika kijiweni uongozi wa kijiwe uliamuru nifungiwe minyororo pikipiki yangu na nilipokataa kulipa gharama hiyo walinipiga marufuku kuendesha pikipiki hiyo Kishili na kama ntaendesha watanichomea pikipiki yangu"
Kwa kuzingatia maelekezo ya serikali ya awamu ya tano inayotaka wananchi wa hali ya chini kujishughulisha bila kusumbuliwa, mkuu wa Wilaya aliwataka viongozi wa kijiwe hicho kufika ofisi yake Ijumaa tarehe 22 Disemba 2019 wakiwa na vielelezo vyote vya kisheria ikiwa ni pamoja na ripoti za fedha, katiba na viambatanisho vingine vinavyoruhusu ukusanyaji huo wa fedha kufanyika.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana yuko katika ziara za kawaida za kikazi katika Wilaya yake akifanya mikutano ya hadhara katika kata zote za wilaya yake akisikiliza kero, malalamiko na ushuri kutoka kwa wananchi.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.