Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Nassoro Makilagi akiambatana na Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, wajumbe wa Kamati ya Siasa wa kata husika, pamoja na wakuu wa Idara husika toka Jiji la Mwanza leo tarehe 10 Julai, 2024 amefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Kata ya Mhandu na Kata ya Mabatini Wilayani Nyamagana ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika Kata 18 za Wilaya hiyo kwa lengo la kuona maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba inakamilika kwa wakati.
Mhe. Makilagi katika ziara hiyo amekagua mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za Kasota (1), Mandu Sekondari (11) na matundu ya vyoo 20, Shule ya Msingi Nyakato A (5), Shule ya Msingi Pamba B (2), Shule ya Msingi Pamba C (2), Shule ya Msingi Mabatini (2) na Shule ya sekondari Mtoni yenye jengo lenye vyumba 16 vinayojengwa kwa kiwango cha ghorofa, vilevile Ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Shigunga na Zahanati ya Mhandu iliyopo katika hatua za ujenzi wa msingi na umekamilika. Pia alizuru eneo jipya jirani na shule ya Msingi Kasota ambapo inatarajiwa kujengwa Shule ya Sekondari Kasota iliyotengewa jumla ya Shilingi Milioni 584.2.
Katika kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Msingi Pamba C iliyoanza ujenzi kwa nguvu za Wananchi, Mhe. Makilagi ametoa mifuko 50 ya saruji, kwa kuungwa mkono na Mkuu wa idara ya Ugavi Ndg. Majili ambae ametoa trip 2 za mchanga, Mhandisi David Nestory trip 1 ya mchanga, Afisa Elimu Bi. Catherine trip 1 na Ndg. Kefa Mchumi wa Jiji trip 2 za mchanga ili kusaidia ukamilishwaji wa madarasa hayo kwakuwa yana hitajika sana kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani katika shule hiyo.
Mhe. Makilagi amesema “Miradi yote hii inayotekelezwa ndani ya Nyamagana inajengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri, hivyo ninatoa rai kwa wote mnaosimamia miradi hii kuwa waaminifu na wazalendo kwa fedha mlizopata na mhakikishe ujenzi unakamilika kwa wakati na majengo yaanze kutoa huduma mara moja ili kupunguza adha ya upungufu wa madarasa kwa shule zenye uhitaji mkubwa wa madarasa na madawati.”
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Mhe.Sima Costantine Sima ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mhandu, amemshukuru Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe. Makilagi kwa ziara hiyo na kusema maagizo yote yaliyotolewa yatayafanyiwa kazi na kwamba atakapo rudi tena katika Kata yake atakuta mabadiliko makubwa.
Akihitimisha ziara hiyo Mhe. Makilagi amewataka viongozi wote wa kata hizo kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa kwa Kata zote za Wilaya ya Nyamagana.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.