Leo tarehe 7/03/2024 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Nassor Makilagi, ameongoza kongamano la wanawake katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kiwilaya katika uwanja wa Nyamagana - Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi (Katikati aliye vaa lemba la bluu) akisheherekea pamoja na wakina mama siku ya Mwanamke Duniani Kiwilaya katika uwanja wa Nyamagana.
Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka tarehe 8, Machi kwa lengo la kupigania harakati za mwanamke katika nyanja ya uchumi, siasa na kijamii. Aidha Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo Mhe.Amina Makilagi amewaeleza wanawake kuwa kupitia kongamano hilo watapata elimu na uelewa wa namna ya kujiinua kiuchumi na kuweza kujipambanua katika majanga yanayoikabili jamii yetu.
Pia amewataka wanawake kusaidiana na Serikali kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuwa wanaofanyiwa vitendo hivyo ni watoto wao hivyo ni muhimu kwa wanawake kusimamia suala la malezi kikamilifu kwa watoto ili kuwa na kizazi imara kitakachokuja kuwa nguvu kazi ya Taifa.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Jiji la Mwanza Ndg.Mariam Mdesa amesema “Mwanamke unapoona na kusikia vitendo vya ukatili na kukaa kimya ni wazi unataka kurudisha nyuma maendeleo yetu, hii ni kutokana na wakinamama wengine kukaa kimya pindi watoto wao wanapofanyiwa vitendo vya ukatili”.
Aliongeza kuwa wakinamama wengi wanajisahau kulea watoto wao na kujikita kwenye shughuli za uchumi, hivyo ni vyema kutenga muda wa kukaa na watoto wao ili kubaini kama kuna vitendo vya ukatili wanafanyiwa na mara wanapo baini vitendo hivyo watoe taarifa katika Serikali ya Mtaa anaoishi, dawati la ustawi Polisi au kupiga simu namba 166 ili kupata msaada wa haraka na kukomesha vitendo hivyo.
Pia wanawake kupitia kongamano hilo wamejadili changamoto za ukatili kwa wafanyakazi wa ndani ambapo mdau kutoka Shirika la Wotesawa Ndg.Renalda Mambo amesema “ni vyema sisi kama wanawake kuhakikisha wafanyakazi wetu wa ndani wanapata mishahara yao kwa wakati na kupunguza vitendo vya ukatili dhidi yao kama vile lugha isiyorafiki, kuwapiga na hata kufumbia macho viotendo kama ubakaji kwani hupelekea wao kuurudisha ukatili huo kwa watoto tunaowaacha nao nyumbani wakati tunapokuwa makazini”.
Katika kuhitimisha kongamano hilo Mhe.Amina Makilagi amesisitiza wanawake kuwajibika ipasavyo katika masuala ya malezi na makuzi ya watoto ili kupinga ukatili dhidi yao, lakini pia amewasisitiza wanawake kukuza ubunifu unaoendana na tekinolojia ili kuleta usawa wa kijinsia katika Taifa hili la Tanzania ili kuongeza uwezo wa wanawake kuzichangamkia fursa zilizopo kwa lengo la kuwainua wawe na uchumi binafsi na siyo kuwa tegemezi.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.