CAMFED CDC Mwanza inaendelea kukuza uwezeshaji wa vijana kupitia mafunzo ya elimu ya biashara, ikiwa na lengo la kuwaandaa kuanzisha na kuendeleza biashara endelevu. Mnamo Novemba 28, 2025, kamati hiyo ilifanya kikao kazi na wanaCAMA waliowasilisha maombi ya kupokea mitaji pamoja na mikopo isiyo na riba. Kikao hiki kililenga kutoa elimu ya msingi kuhusu biashara kabla ya vijana kupokea mitaji, ili kuhakikisha uwekezaji watakaoufanya unakuwa wa tija na wenye uwezo wa kubadilisha maisha yao.
Katika kufanikisha shughuli hii, kikao kilihusisha wadau mbalimbali muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Washiriki hao ni pamoja na Mratibu wa Shirika la CAMFED, Afisa Biashara, Afisa Mipango, Afisa Elimu Kata, Mkuu wa Shule, Mwalimu Mlezi na Mwakilishi wa Vikundi vya Wazazi. Ushirikiano wa wadau hao umewezesha vijana kupata elimu sahihi na ya kina kuhusu misingi ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara.
Awali, Kamati ya Maendeleo ya CAMFED (CDC – Mwanza) ilikutana kujadili hatua mbalimbali za utekelezaji wa programu za elimu na uwezeshaji wa wasichana pamoja na kupanga mwelekeo wa mwaka 2026.
Katika kikao hicho, wajumbe walipitia taarifa za ufuatiliaji shuleni kwa mihula miwili na kubainisha mafanikio, changamoto pamoja na maeneo ya kuboresha.
Pia walijadili mpango wa ununuzi wa vifaa vya wanafunzi kwa mwaka 2026 na kumchagua mzabuni wa kusambaza vifaa hivyo.Kupitia mchango wa wataalamu wote waliohudhuria kikao cha leo, vijana wamepata fursa ya kujifunza kuhusu usimamizi wa fedha, mbinu za kukuza biashara, misingi ya ujasiriamali na matumizi sahihi ya mitaji watakayopokea. Mafunzo haya yanawasaidia kupanga vizuri shughuli zao za kiuchumi na kuwekeza kwa umakini ili kupata matokeo ya muda mrefu.
Kwa jumla, vijana 33 wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya mitaji, huku vijana 3 wakipatiwa mafunzo kwa ajili ya mikopo isiyo na riba. Mafunzo haya yamefanyika katika ofisi za CAMFED zilizopo katika Shule ya Sekondari Mtoni jijini Mwanza. Hatua hii inaendelea kuthibitisha dhamira ya CAMFED ya kuwawezesha vijana, hasa wasichana, kupitia elimu, kipato na uhuru wa kiuchumi.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.