Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Jiji la Mwanza limepokea, kujadili na kupitisha mapendekezo ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya shilingi 124,378,085,328,00 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi ambacho ni maalumu kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya bajeti kiliongozwa na Kaimu Mkurugenzi Bw. Peter Lehhet ambaye ni Mkuu wa Idara ya Tehama January
29, 2025 katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri.
Bw. Lehhet amefafanua na kueleza kuwa kikao hicho ni maalumu kwa ajili ya kupitia,kujadili na kufanya tathmini ya utendaji kazi ambapo kila mfanyakazi ana haki katika utekelezaji wa majukumu na stahiki anapowajibika kutimiza malengo yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha rasimu ya Bajeti ya mwaka 2025/2026 kwa niaba ya Mkurugenzi Bw. Jeremiah Lubeleje ambaye ni Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri amefafanua kuwa Halmashauri inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Tsh124,378,085,328.00 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo.
Bw. Lubeleje amefafanua mchanganuo wa fedha hizo zinazokadiliwa katika Bajeti hiyo kuwa kiasi cha shilingi 83,006,538,000.00 ni fedha ya mishahara ya Watumishi, Kiasi cha Shilingi 2,443,743,000.00 ni matumizi ya kawaida (OC), Kiasi cha Shilingi 6,065,121,084.00 ni Ruzuku ya miradi ya maendeleo, Kiasi cha Shilingi 3,936,058,000.00 ni fedha kutoka kwa wahisani/wadau wa maendeleo na Shilingi 28,926,625,244.00 ni fedha zitokanazo na vyanzo vya Mapato ya ndani ya Halmashauri.
Nao wajumbe wa Baraza la wafanyakazi waliipongeza Ofisi ya Mipango na Uratibu kwa mpangilio mzuri wa Bajeti hiyo na walipata nafasi ya
kupitia, kujadili na kutoa maoni yao juu ya
Bajeti hiyo na mwisho kwa kauli moja waliriidhia na kuipitisha bajeti hiyo.
Aidha Lubeleje ameeleza kuwa pamoja na kuwepo kwa rasimu ya bajeti hiyo ofisi ya Mipango na Uratibu imeahidi kutekeleza na kufanyia kazi mapendekezo na maazimio ya kikao hicho ikiwa ni pamoja na kuendeleza ushirikiano na kuboresha huduma za kijamii, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, na kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi kupitia maslahi bora na mazingira ya kazi.
Akihitimisha kikao hicho Kaimu Mkurugenzi aliwashukuru wajumbe wote kwa kushiriki,kutoa mapendekezo na kuridhia kupitisha rasimu hiyo ya bajeti na kuwahakikishia wajumbe kuwa atasimamia na kufanyia Kazi mapendekezo yote ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi katika utendaji wa kila siku.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.