Katika jitihada za kuhakikisha utendaji kazi wa Mabaraza ya kata unaimarika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya jiji la Mwanza, leo Machi 26,2025 Wenyeviti, makatibu na wajumbe 131 wameapishwa na kukumbushwa majukumu yao.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi mkubwa wa Jiji na kuhudhuriwa na Maafisa Sheria wa Halmashauri ambao kabla ya kuwaapisha wajumbe waliwaelimisha namna ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usuluhishi katika mabaraza ili kumaliza migogoro katika jamii.
Awali Bw. Nobert John Sospeter Afisa Sheria, aliwakumbusha wajumbe juu ya sheria za uundaji wa Mabaraza ya Kata, muundo, sifa za mtu kuwa mjumbe wa Baraza pamoja na kuwakumbusha majukumu ikiwa ni namna ya utekelezaji wa majukumu hayo.
Aidha Wakili Mwandamizi wa Serikali Richard Vungwa alipata nafasi ya kuwaapisha wajumbe hao na kuwataka kutenda haki wakati wakitimiza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo.
Wakili Vungwa aliitaja migogoro itakayoshughulikiwa na Mabaraza hayo kuwa ni pamoja na migogoro ya ndoa na migogoro ya ardhi.
Sambamba na hilo amewataka wajumbe kuwa wasuluhishi na siyo waamuzi,kwani kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama ya Migogoro ya Ardhi sura ya 216, mabaraza ya kata yanasikiliza Migogoro na kusuluhisha na ikishindikana baraza litatoa hati ya kushindikana usuluhishi wa mgogoro kwa hatua zaidi.
Mabaraza ya kata ni vyombo vilivyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha Sheria ya mabaraza ya kata ya mwaka 1985, ambapo kila baraza linajumuisha wajumbe wasiopungua wanne na wasiozidi wanane watakaochaguliwa na kamati ya kata kutoka miongoni mwa majina ya wakazi wa kata yaliorodheshwa kwa kuzingatia taratibu maalum uliowekwa.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.