Kamati ya Afya ya Msingi ya Jiji la Mwanza imejadili juu ya suala la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ulio ripotiwa na Daktari Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dr. Pima Sebastian siku ya tarehe 9 Januari,, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akitoa taarifa ya uwepo wa ugonjwa huo wa kipindupindu katika kikao hicho kilicho jumuisha wadau mbalimbali kama MWAUWASA, TARURA, TMDA, Watendaji wa kata, na baadhi ya wenyeviti, Daktari Pima amesema " Mnamo tarehe 04 Januari, 2024 tumepokea wagonjwa wawili wenye dalili za ugonjwa wa kipindupindu ambao walitokea Mkoa jirani wa Simiyu ambako walienda kwa shughuli za msiba. Walianza kusikia dalili za kuharisha na walipofika Igoma walipokelewa katika Zahanati ya Igoma na kuchukiliwa sampuli nazo zilibainika kuwa na ugonjwa huo baadaye walipelekwa katika kituo cha matibabu kilichopo mkuyuni."
Aidha, amesema kuwa zimeendelea kulipotiwa taarifa za visa vingine vya ugonjwa huo viwili toka eneo la Mkolani, vitatu Wilaya ya jirani ya Ilemela na hadi sasa kuna jumla ya wagonjwa 7 waliolazwa na wawili wameruhusiwa wanaendelea vizuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wenyeviti Ndg. Abubakar Ameshauri kuwa taarifa hizi za mlipuko wa kipindupindi zisambazwe ziwafikie wananchi kupitia mitandao ya kijamii kwenye makundi ya wenyeviti, watumishi, wanamichezo, na watumishi wasio wa umma.
Naye Mhe. Diwani wa kata ya igoma Ndg. Musa Ngolo amesisitiza kuwa elimu ya njia sahihi ya kujikinga na kipindupindu itolewe bila kuyasahau makundi maalumu kama wasio sikia na wasio ona pia kuwepo na mawasiliano ya haraka toka eneo husika waliko patikana wagonjwa ili hatua za haraka zichukuliwe ili kuzuia maambukizi zaidi.
Mwenyekiti wa kamati ya Afya ya Msingi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Ndg. Thomas James Salala amesisitiza kuwa taarifa zianze kutolewa mara moja kwa jamii juu ya uwepo wa ugonjwa huu kupitia vyombo vya habari, matangazo ya barabarani, na vikao vya mitaa ili kuhamasisha watu namna ya kujikinga kwa pamoja tuepukane na mlipuko huu wa ugonjwa wa kipindupindu.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.