Mkuu wa wilaya ya Nyamagana mheshimiwa Mary Tesha ameanza ziara ya kikazi jana kukagua shule za sekondari zilizopo Jijini Mwanza.
Katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya aliambatana na Kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya,pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Mkuu wa wilaya alifanikiwa kutembelea shule ya sekondari Fumagila,Igoma na Shamaliwa.
Katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya amebaini upungufuwa madawati na madarasa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza kulingana na sera ya serikali ya awamu ya Tano ya “elimu bila malipo”
Sera hii imehamasisha wananchi kuwapeleka watoto shule na kuzifanya shule zetu kuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi.
Aidha katika ziara yake hiyo Mheshimiwa Tesha akiwa katika shule ya sekondari Shamaliwa amewataka wanafunzi wa kike kupimwa ujauzito mara kwa mara ili kuweza kuwabaini wanafunzi wajawazito “serikali haina mzaa hata kidogo na watoto wanaopata mimba shuleni wakati serikali inaangaika kuwasomesha” amesema Bi Tesha.
Wakati huo huo Mkuu wa wilaya akiwa shule ya sekondari ya Igoma amechangia kiasi cha Tsh 500,000 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya choo katika shule hiyo
Aidha Mkuu wa wilaya amehamasisha jamii kuchangia kwa hiyari maendeleo ya shule hizo kutokana na upungufu uliopo licha ya jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya Tano kuboresha elimu.
Ziara hii ni utaratibu wa kikazi aliojiwekea Mkuu wa wilaya wa kutembelea miradi ya maendeleo. Mkuu wa wilaya ataendelea kukagua shule za sekondari ambazo zipo zaidi ya 50.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.