Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Nassoro Makilagi leo tarehe 25/01/2024 ameongoza kikao mkakati cha kutokomeza mlipuko na maambukizi mapya ya ugonjwa wa kipindupindu katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, kilicho jumuisha Mganga Mkuu wa Serikali, wakuu wa Idara mbalimbali ndani ya Jiji, walimu wakuu Shule za Msingi na Sekondari, Watendaji wa Kata na Mitaa, maafisa afya, maendeleo ya jamii, wataalam wa kilimo, mifugo na uvuvi, na kamati ya usalama ya Wilaya.
Akifungua kikao hicho Mhe. Makilagi amesema " Lengo kubwa leo tufanye tathimini ili tujuwe tangu ugonjwa wa kipindupindu umeanza hadi sasa hali ikoje na kwamba kufikia tarehe 27/01/2024 pasiwepo ugonjwa huu tena. " Amesema Mhe. makilagi.
Akitoa tathimini hiyo kwa niaba ya Daktari wa Wilaya Ndugu Sophia Kiluvya ambaye ni Afisa Afya wilayani hapa amesema kuwa tangu ugonjwa huu umeingia wilayani Nyamagana tumepokea wagonjwa 66. Wagonjwa 06 wakiwa wametokea Wilaya jirani na wagonjwa 60 kutoka wilaya ya Nyamagana. Ambapo hadi sasa wagonjwa 62 wameruhusiwa , wawili (02), na wawili walifariki.
Mhe. Makilagi amemkaribisha Mganga mkuu wa serikali profesa. Nagu katika kikao hicho huku akimshukuru kwa kuwa tayari kufika mwanza hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kuwatia moyo wauguzi lakini pia kushauri ili kusaidia kuzuia ugonjwa huu Nyamagana na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla.
Kwa upande wake Profesa. Nagu ameshukuru kuwa sehemu ya kikao hicho na kuwasilisha salaam za pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na watendaji wake wote hasa sekta ya Afya kwa kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa na kuhakikisha Afya zao zinaendelea kuboreka.
Profesa Nagu amesema "Ugonjwa wa kipindupindu ni ugonjwa wa uchafu hivyo sisi watumishi tuhakikishe maeneo yetu ya makazi , biashara maeneo ya kazi na mazingira yote kwa ujumla ni safi ili vimelea vya ugonjwa huu visiendelee kukua, na mitaro yote yenye changamoto izibuliwe pamoja na maeneo ya wavuvi na jamii kwa ujumla.
Aidha Profesa Nagu amewasihi watumishi wote kuhakikisha wanahamasisha usafi na matumizi sahihi ya vyoo pamoja na kuweka miundombinu bora katika maeneo ya vyoo ili kila mtu anapomaliza kupata huduma ya haja ndogo na kubwa anawe mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Akihitimisha kikao hicho Mhe. Makilagi amesema kuwa kutokana na mikakati hii na maelekezo haya, mtaa utakao ripotiwa kuwa bado una ugonjwa wa kipindupindu baada ya tarehe 27/01/2024 kila anayehusika katika eneo hilo ataandika barua ya mistari mitatu(3) akieleza kwa nini yeye aendelee kuwa mtumishi wa serikali ya Tanzania.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.