Katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika leo Disemba 09,2024 Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeadhimisha sherehe hizo kwa kupanda miche ya miti ya matunda na vivuli zaidi ya 500 na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira pamoja na Michezo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema katika kuadhimisha siku hiyo wamepanda miti katika shule mpya ya Msingi Shadi inayojengwa Kata ya Luchelele, shule ya msingi Buhongwa na Bulale Sekondari ambapo miti hiyo itasaidia kupata mvua za kutosha, kupunguza mafuriko, kusaidia kukabiliana na ukame pamoja na kupunguza hewa chafu ya ukaa inayoweza kuathiri mazingira na Afya za binadamu.
Makilagi ameongeza kuwa zoezi la usafi limefanyika maeneo mbalimbali Katika jiji la Mwanza ikiwemo Hospital ya Wilaya ya Nyamagana (Butimba) ambapo amesisitiza zoezi hili kuwa endelevu ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi kwa ulinzi wa Afya za wananchi wanaoishi katika maeneo husika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Bi Agnes Majinge ambaye ni Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza amesema kuwa katika kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru Sekta ya Michezo imepiga hatua kubwa kupitia Serikali ya awamu ya sita na kumpongeza Mhe Rais kwa namna anavyojitoa na kuhakikisha Michezo inasonga mbele hasa kupitia goli la mama.
Hivyo nasi kwa kutambua umuhimu wa Michezo Mkurugenzi wa Halmashauri ameandaa mashindano ya mechi kati ya timu ya Mwanza Veteren na Mwanza City Council Veteran ambazo zimecheza katika maadhimisho hayo na kuwaomba wadau wa Michezo kujitoa kwa hali na Mali ili kuwawezesha wachezaji na vijana chipukizi waendelee kukuza vipaji vyao na sekta ya Michezo kwa ujumla.
Bi Agnes amehitimisha kwa kusema kuwa Michezo ni Afya na kuwataka wananchi kushiriki mazoezi ya mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha Afya zao.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.