"Nimeridhishwa na kasi ya ujenzi pamoja na vifaa vya kisasa vinavyotumika kwenye ujenzi huu" Mhe Mwanaidi Ali Khamis
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ametoa kauli hiyo Januari 09.2021 akiwa kwenye ziara ya siku moja katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kukagua mradi mkakati wa ujenzi wa Soko Kuu uliopo Kata ya Pamba katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza utakaogharimu Shilingi Bilioni 23
Mhe. Khamis akiwa ameambatana na wenyeji wake Dkt. Philis Nyimbi Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na kamati yake ya Ulinzi na usalama, amekagua ujenzi wa soko Hilo la Kisasa uliofikia 8% ya ujenzi wake na kuridhishwa na telnolojia yenye mitambo ya kisasa inayotumiwa na mkandarasi mzawa wa kampuni ya ujenzi ya Mohammed Builders.
Aidha Mhe. Khamis ameagiza Mkandarasi Mshauri kuweka usimamizi wa mradi huo kwa masaa 24 sanjari na kutoa siku mbili kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kusimamia Mkandarasi aweke mpango madhubuti wa utatuzi wa uhaba wa Saruji ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nyamagana Mhe. Stanslaus Mabula ameishukuru serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli kutoa fedha ili mradi huo utekelezwe ambao ujenzi wake ulisitishwa kwa taratibu kadhaa za kiserikali takribani mwaka mmoja ambao ulileta adha kwa wananchi wanaohitaji huduma pamoja na wafanyabiashara na wachuuzi wa Soko Hilo.
Mstahiki Meya wa halmashauri Jiji la Mwanza Mhe. Sima Constantine Sima akiwa ameambatana na wataalamu wa Jiji wakiongozwa na Mkurugenzi wa Jiji Kiomoni Kibamba, kwaniaba ya Halmashauri Jiji la Mwanza ameahidi kuendelea kusimamia vyema miradi mikakati yote inayotekelezwa katika halmashauri yake ambayo itachochea ukuaji wa Jiji la Mwanza pamoja uongezaji wa mapato wa halmashauri ili ijiendeshe yenyewe. Wakati huo huo Mhe. Ngoye Diwani Kata ya Pamba ambaye pia Ni Naibu Mayor ameishukuru serikali kwa ujenzi wa Soko hilo katika Kata yake ya Pamba ambao umesogezea wananchi wake huduma karibu na kuleta unadhifu wa mji.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya Mohammed Builders kampuni ya Kizawa iliyoshinda Zabuni ya ujenzi huo amesema anakutana na wakati mgumu wa utekelezaji wa mradi huo kutokana na uhaba wa Saruji japo Kama analipa fedha kwa wakati viwandani. Hivyo ameiomba serikali itafute namna Bora ya utatuzi wa uhaba huo ili miradi huweze kukamilika kwa wakati.
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.