Wananchi wa Mtaa wa Maswa Mashariki, Kata ya Mhandu jijini Mwanza wamefurahishwa na ujenzi wa barabara ya Ndama inayojengwa kwa mawe yenye urefu wa mita 400 katika Mtaa huo ambayo itasaidia kuondokana na kero mbalimbali walizokuwa wakizipata kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Wameyasema hayo Julai 09, 2022 wakati wa ziara ya Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine iliyolenga kukagua ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni kiunganishi muhimu kutokea eneo la Ndama barabara kuu ya Nyerere.
Anna Kampala ni mkazi wa Mtaa wa Maswa Mashariki, amesema barabara hiyo imekuwa mbovu kwa takribani miaka 50 hali ambayo ilikuwa ikisababisha adha kubwa hususani msimu wa mvua.
"Wakati wa mvua hali ilikuwa ni mbaya zaidi kwani maji yalikuwa yakituama na kutengeneza mabonde, wagonjwa walikuwa wanapata shida kufika hospitalini sanjari na wazazi kujifungulia njiani, lakini kwa sasa shida zote hizo zitakuwa ni historia" amesema Kampala
Kwa upande wake Edward John ambaye pia pia ni Mkazi wa Mtaa wa Maswa Mashariki amesema kukamilika kwa barabara hiyo Kitasaidia makazi yao kuwa na thamani na kuongeza idadi ya watu watakaokuwa wanaitumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Maswa Mashariki, Rashid kabazi ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo wameiangalia barabara hiyo kwa jicho la pili kwani wananchi walikuwa wanapata changamoto wakati wa kupita kwenda sehemu mbalimbali.
Nao baadhi ya mafundi wanaotekeleza mradi huo akiwemo Hamadi Suleiman wamesema wanakutana na changamoto ya wananchi kupita wakati ujenzi unaendelea na hivyo kukwamisha juhudi za kukamilisha ujenzi mapema.
Mradi huo utagharimu zaidi ya milioni 234 na unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki moja kuanzia sasa.
Serikali inazidi kufanya kazi kubwa ya utatuzi wa kero mbalimbali katika sekta ya miundombinu kwa kutoa fedha za kujenga barabara mpya na kukarabati barabara zmbalimbali na Kata ya Igoma, Mhandu tumekuwa wanufaika wa fedha hizo.
Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Rasu Contractor utawanufaisha wakazi wa Mitaa zaidi ya minne na ni mfululizo wa miradi ya barabara inayoendelea kutekelezwa katika Kata ya Mhandu jijini Mwanza
Barabara ya Balewa
Sanduku la Posta: 1333,Mwanza
Simu: +255 28 250 1375
Simu ya Kiganjani: 0755741738
Barua Pepe: cd@mwanzacc.go.tz
Copyright ©2017 Mwanza City Council . All rights reserved.